1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Jimmy Lai atunukiwa tuzo ya Uhuru wa Kujieleza ya DW 2026

1 Mei 2026

Mchapishaji ambae pia mpigania demokrasia wa Hong Kong, Jimmy Lai, ametunukiwa tuzo ya heshima na DW.

Mjasiriamali wa vyombo vya habari na mwanaharakati wa demokrasia Jimmy Lai
Mjasiriamali wa vyombo vya habari na mwanaharakati wa demokrasia Jimmy Lai.Picha: Alex Ogle/AFP

Kabla ya kufungwa kifungo cha miaka 20 gerezani, Jimmy Lai alianzisha gazeti kubwa zaidi la Hong Kong linalopigania demokrasia. Mwanawe amesema kuwa tuzo hiyo inaonyesha kwamba wale wanaopigania uhuru wa wengine "hawako peke yao kamwe.”

Akiwasili Hong Kong akiwa na umri wa miaka 12 bila hata senti moja, baada ya kusafiri kwa kujificha kutoka kusini mwa China, Jimmy Lai alikuwa akitafuta tu uhuru na mustakabali wa maisha yake. Wakati huo, Lai hangeweza kamwe kufikiria namna ambavyo maisha yake yangefungamana moja kwa moja na koloni hilo la zamani la Uingereza.

"Nitazama pamoja na meli, kwa sababu mahali hapa pamenipa kila kitu,” Lai alisema katika mahojiano kuhusu Hong Kong na DW miezi michache kabla ya kukamatwa kwake mwezi Desemba 2020. Alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza maarufu kulengwa chini ya "sheria ya usalama wa taifa” iliyowekwa Hong Kong na Beijing baada ya ukandamizaji wa maandamano ya kupigania demokrasia.

Beijing ilikuwa imesema kuwa sheria hiyo ingerejesha Hong Kong "kutoka katika machafuko hadi katika utaratibu,” baada ya maandamano ya mwaka 2019 dhidi ya muswada wa kuruhusu watuhumiwa kurejeshwa China kubadilika na kuwa maandamano makubwa dhidi ya Beijing kwa kuingilia uhuru wa kiraia wa Hong Kong.

Tangu wakati huo, tajiri huyo wa vyombo vya habari anayeunga mkono demokrasia amedumu kwa takribani siku 2,000 katika kifungo chenye upweke mkubwa ndani ya Gereza lenye usalama wa hali ya juu la Stanley huko Hong Kong.

Kesi ya Lai iliyodumu kwa miaka mingi ilimalizika mwezi Februari huu, ambapo mzee huyo mwenye umri wa miaka 78 alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la "kushirikiana na nguvu za kigeni.” Ingawa alikuwa amekana mashtaka yote, huku timu yake ya wanasheria ikisema kuwa hatawasilisha rufaa.

Hukumu hiyo ndiyo adhabu kali zaidi kuwahi kutolewa chini ya sheria ya usalama wa taifa, na kesi ya Lai kwa wengi imekuwa alama ya kudidimia kwa kiasi kikubwa kwa uhuru wa vyombo vya habari huko Hong Kong, kama sehemu ya mkakati mpana wa Beijing wa kunyamazisha sauti zinazokosoa.

Jimmy Lai ametambuliwa na DW

Kwa kutambua mchango wake katika kutetea uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza, DW imemtunuku Jimmy Lai tuzo ya mwaka huu ya Freedom of Speech Award.

Barbara Massing, Mkurugenzi Mkuu wa DW, akizungumza katika mahojiano ya TVPicha: DW

Tangu mwaka 2015, Tuzo ya DW ya Uhuru wa Kujieleza imekuwa ikiwatunuku waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu kama njia ya kuangazia vikwazo dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na hali zinazotia wasiwasi kuhusu haki za binadamu kote duniani.

Sebastien Lai, mtoto wa Jimmy Lai na mtetezi wa muda mrefu wa kuachiwa kwake, aliiambia DW kuwa "watu wanaopigania uhuru, wa wengine hawako peke yao kamwe.” Aliongeza kuwa hili ni jambo la maana hasa katika wakati ambapo "vyombo vingi vya habari nchini Hong Kong sasa vinajifanyia udhibiti binafsi.”

"Nadhani kama angefahamu kuhusu tuzo hiyo, angefurahi sana,” Sebastien Lai alisema. Mkurugenzi Mkuu wa DW, Barbara Massing, amesema kuwa kupitia tuzo hiyo, DW inamheshimu Jimmy Lai kwa "kujitolea kwake kusiko na mbadala katika kutetea maadili ya kidemokrasia.”

Amesema Jimmy Lai amesimama bila kuyumba kutetea uhuru wa vyombo vya habari nchini Hong Kong, akichukua hatari kubwa binafsi, hata wakati nafasi ya uandishi wa habari huru ikiendelea kupungua. Kupitia Apple Daily, aliwapa waandishi wa habari jukwaa la kuripoti kwa uhuru na kuipa sauti harakati za demokrasia nchini Hong Kong.

Na kuongeza kuwa msimamo wake unakumbusha ulimwengu kwamba kwamba uhuru wa vyombo vya habari hauji wenyewe  ni kitu kinachopaswa kutetewa kila wakati.

Je, Jimmy Lai ataweza kuachiliwa huru?

"Hukumu ya miaka 20 ni sawa na hukumu ya kifo,” alisema Sebastien Lai. Familia yake ina wasiwasi mkubwa kuhusu afya ya mzee huyo mwenye umri wa miaka 78 akiwa gerezani, wakisema Jimmy Lai ana ugonjwa wa kisukari, amepungua kilo 10 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, na pia anakabiliwa na matatizo ya kucha kung'oka na meno kuoza.

Sebastien hajamuona baba yake kwa miaka mitano na wanaweza kuwasiliana tu kwa njia ya barua. Hawezi kurejea Hong Kong kwa sababu za kiusalama. Alisema inaumiza sana kujua kwamba "kuna uwezekano mkubwa sana kwamba Jimmy Lai atafariki akiwa gerezani.”

Clifford, ambaye amemfahamu Jimmy Lai kwa zaidi ya miaka 30, alionya kuwa kumwacha Lai afie gerezani kutakuwa "maafa” kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) na kutamfanya kuwa mfungwa wa pili wa kisiasa mwenye hadhi ya juu kufia akiwa kizuizini nchini China, baada ya mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Amani Liu Xiaobo, aliyefariki kwa saratani mwaka 2017.

Upande wa mashtaka, hata hivyo, umenukuu ripoti za kitabibu zinazoeleza kuwa hali ya afya ya Lai iko "tulivu.” Umekataa madai ya kudorora kwa afya yake, ukisema kuwa alizuiliwa kwa kifungo cha upweke kwa ombi lake mwenyewe kwa sababu za kiusalama.

Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye mwaka 2025 alisema alimwomba kiongozi wa China Xi Jinping "azingatie” kumuachilia Lai, anatarajiwa kukutana tena na Xi mjini Beijing mwezi ujao.

Sebastien Lai alisema ana matumaini kuwa Trump anaweza kuingilia kati na kusaidia kuachiwa kwa baba yake, akizingatia "rekodi yake ya kipekee ya kuwatoa watu gerezani.”

Hata hivyo, aliongeza kuwa kwa wakati huu ni vigumu kuwazia itakuwaje endapo baba yake ataachiwa huru. "Hata kukaa tu mezani nyumbani kwetu, kupika chakula na familia yote kula pamoja. Nafikiri hilo ndilo jambo ninalolitamani zaidi.”

Kupanda meli kwa siri hadi tajiri wa vyombo vya habari

Jimmy Lai alizaliwa katika familia tajiri huko Guangzhou, mji ulioko kusini mwa China. Maisha yake yalivurugika kabisa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya China. Baba yake alikimbia nchi, mama yake alipelekwa katika kambi ya kazi ya lazima, na familia yao ikapoteza kila kitu.

Akiwa na umri wa miaka 12, baada ya kuonja kipande cha chokoleti kutoka Hong Kong ladha adimu aliyodhani ilitoka kwenye ulimwengu bora zaidi Lai aliamua kupanda kwa siri katika mashua ya wavuvi iliyokuwa ikielekea huko katika koloni la Uingereza, ambalo baadaye lilikabidhiwa kwa China mwaka 1997.

Katika Hong Kong ya miaka ya 1960, akianzia na mikono mitupu, Lai aliendelea kuwa tajiri mkubwa wa biashara ya nguo kupitia mafanikio ya chapa yake ya mavazi, Giordano, iliyoanzishwa mwaka 1981. Kwa Lai, uhuru mwanzoni ulimaanisha shibe, lakini baada ya kufikia usalama wa kifedha, alitambua kuwa uhuru ulikuwa na maana pana zaidi.

Mauaji ya waandamanaji wa kudai demokrasia katika Uwanja wa Tiananmen mwaka 1989 mjini Beijing yalikuwa hatua ya mabadiliko makubwa katika maisha yake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW