1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchekeshaji Volodymyr Zelensky ashinda urais Ukraine

Yusra Buwayhid
22 Aprili 2019

Mchekeshaji asiye na uzowefu wa kisiasa, Volodymyr Zelensky, ameshinda ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa rais nchini Ukraine Jumapili, na kupongezwa na viongozi duniani kote.

Ukraine, Kiew: Wolodymyr Selenskyj
Picha: picture-alliance/dpa/Stringer

Matokeo hayo yanaangaliwa kama maamuzi ya raia waliochoshwa na ufisadi uliotawala katika taifa hilo, pamoja na hali duni ya maisha.

Zelensky ambaye uzowefu wake pekee wa kisiasi ni kuigiza kama rais katika kipindi cha televisheni, amemshinda rais aliyekuwa madarakani Petro Poroshenko kwa kunyakua asilimi 73 ya kura zote zilizopigwa, kulingana na matokeo rasmi ambayo hayakukamilika.

Poroshenko amepata asilimia 24 ya kura, na kupoteza madaraka kwa Zelensky mwenye umri wa miaka 41, huku asilimia 42 ya masanduku ya kura yakiwa yameshahesabiwa.

Na matokeo ya kustaajabisha ikizingatiwa jinsi kampeni yake ilivyoanza kama mchezo tu, lakini bila kutegemea ujumbe wake uliwavutia wananchi wa Ukraine ambao wamechoshwa na udhalimu katika jamii, ufisadi na vita vya mashariki mwa nchini hiyo kati ya serikali na waasi wanaotaka kujitenga ambao wanaungwa mkono na Urusi. Vita hivyo vinatajwa kusababisha vifo vya wapatao 13,000.

'Kamwe sitowaangusha'

Nyota huyo wa mchezo wa kuigiza wa televisheni kwa jina la "Mtumishi wa Watu", sasa atakamata hatamu ya madaraka na kuliongoza taifa lenye idadi ya watu wapatao milioni 45.

"Kamwe sitowaangusha," Zelensky amewaambia wafuasi wake waliokuwa na furaha akiwa katika makao makuu ya kampeni yake.

Petro Poroshenko kushoto, na Volodymyr Zelensky kulia

"Ninaweza sasa kuziambia zile nchi zote zilowahi kuwa ya Kisovieti: 'Tuangalieni sisi! Chochote kile kinawezekana!'," amesema Zelensky.

Matamshi hayo huenda mlengwa ikawa nchi jirani ya Urusi, ambako Rais wake Vladimir Putin aliyepo madarakani kwa zaidi ya miaka 2o na wengine wengi wamekuwa wakiufwatilia uchaguzi huo kwa ukaribu.

Pongezi duniani kote

Pongezi za ushindi wa Zelensky, zilimiminika kutoka barani Ulaya na kwengineko. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na wa Poland Andrzej Duda wamempongeza kwa njia ya simu rais huyo mteule.

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO Jens Stolenberg na Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk wamesema wanategemea kuendeleza ushirikiano kati yao.

"Tunampongeza Rais-mteule Volodymyr Zelensky," umeandika Ubalozi wa Marekani Ukraine katika ukurasa wake wa Twitter.

Kampeni ya urais ya Zelensky haikuwa na mihadhara ya kijadi, badala yake mchekeshaji huyo alikuwa na hafla za vichekesho, pamoja  na kuwavutia wapiga kura kupitia mitandao ya kijamii.

Poroshenko amesema, matokeo ni ya wazi na ni sababu tosha ya kumpigia simu mshindani wake na kumpongeza.

Chanzo (afp,ap)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW