1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiAfrika

Mchungaji Paul Mackenzie ashtakiwa kwa mauaji Kenya

13 Agosti 2024

Kiongozi wa dhehebu la njaa nchini Kenya amefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mauaji ya bila kukusudia, kuhusiana na vifo vya watu zaidi ya 400. Mackenzie aliwahubiri waumini kujiua kwa njaa ili wakutane na Yesu.

Kenya|  Mombasa|  Paul Mackenzie
Mchungaji Mackenzie aliwahimiza waumini wake kufunga hadi kufa ili wakutane na bwana Yesu Kristo mbinguni.Picha: Halima Gongo/DW

Mchungaji Paul Nthenge Mackenzie na washukiwa kadhaa walikanusha kuwa na hatia mnamo Januari kwa makosa kadhaa ya kuua bila kukusudia, katika mmoja ya kesi kadhaa dhidi yao kuhusu kile kinachojulikana kama "Mauaji ya Msitu wa Shakahola".

Mackenzie alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi katika mji wa bandari ya Bahari ya Hindi wa Mombasa pamoja na washukiwa wengine 93, waendesha mashtaka na maafisa wa mahakama walisema.

"Hakujawahi kutokea kesi ya mauaji kama hii nchini Kenya," mwendesha mashtaka Alexander Jami Yamina aliiambia AFP, akiongeza kwamba watafunguliwa mashtaka chini ya sheria ya Kenya inayohusika na mikataba ya kujitoa mhanga. "Hii itakuwa kesi ya kipekee ya mauaji bila kukusudia."

Mackenzie anadaiwa kuwachochea wafuasi wake kufa kwa njaa ili "kukutana na Yesu" katika kisa kilichozua taharuki nchini Kenya na kote duniani.

Soma pia: Mahakama nchini Kenya yatishia kumwachia huru Paul Mackenzie

Alikamatwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya miili kadhaa kugunduliwa kwa mara ya kwanza katika msitu wa Shakahola ulioko bara kutoka mji wa Bahari ya Hindi wa Malindi.

Mchungaji Paul Mackenzie, kushoto, akiwa mahakamani mjini Mombasa.Picha: Halima Gongo/DW

Waokoaji walitumia miezi mingi kupekua eneo hilo na sasa wamefukua karibu miili 448 kutoka kwenye makaburi ya halaiki.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa wengi wa waathiriwa walikufa kwa njaa. Lakini wengine, wakiwemo watoto, walionekana kunyongwa, kupigwa au kuzuwiliwa pumzi.

Nyaraka za awali za mahakama pia zilisema kuwa baadhi ya miili hiyo ilitolewa viungo vyao.

Mashahidi zaidi ya 400

Hati ya mashtaka inaorodhesha washtakiwa 95 -- wanaume 55 na wanawake 40 akiwemo mke wa Mackenzie.

Lakini mwanamke mmoja aliyeshtakiwa alifariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi kutokana na "matatizo yanayohusiana na ugonjwa wa muda mrefu na athari za njaa," Yamina aliiambia AFP, na kuongeza kuwa alifariki "mwezi mmoja au zaidi uliopita".

Takriban mashahidi 420 wametayarishwa na waendesha mashtaka, huku kesi hizo zikipangwa kusikilizwa kwa siku nne hadi siku ya Alhamisi. "Kutokana na uzito wa kesi hiyo, tumejiandaa vyema," alisema Yamina.

 Baadhi ya mashahidi watawasilisha ushahidi wao kwa faragha.

Soma pia: Washukiwa mauaji ya Shakahola waendelea kusota rumande

Washukiwa hao walifikishwa mahakamani mwezi uliopita kwa tuhuma za ugaidi kuhusu mauaji ya Shakahola, na pia wanakabiliwa na kesi tofauti za mauaji na mateso ya watoto na ukatili kuhusiana na vifo hivyo. Waendesha mashtaka wanasema haya yalitokea katika kipindi cha 2020 hadi 2023.

Wanafamilia wakilia baada ya kupokea mwili wa ndugu yao ambaye ni muathirika wa dhehebu la njaa katika hospitali ya Malindi, Machi 26, 2024.Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Machi mwaka huu, mamlaka ilianza kutoa miili ya baadhi ya waathiriwa kwa ndugu zao waliokuwa wamechanganyikiwa baada ya miezi kadhaa ya kazi kubwa ya kuwatambua kwa kutumia vinasaba -- DNA. Hadi sasa maiti 34 zimekabidhiwa kwa ndugu.

Maandalizi ya mwisho wa dunia

Mackenzie alikuwa ameanzisha Kanisa lake la Good News International Church mwaka wa 2003, lakini akasema alilifunga mwaka wa 2019 na kuhamia Shakahola kujiandaa na kile alichotabiri kuwa mwisho wa dunia Agosti mwaka jana.

Kisa hicho cha kuogofya kiliisukuma kuweka udhibiti mkali wa madhehebu tofauti, huku maswali yakiibuka kuhusu jinsi Mackenzie alivyoweza kukwepa wasimamizi wa sheria licha ya historia yake ya itikadi kali na kesi za kisheria zilizomkabili hapo awali.

Soma pia: Kenya kuugeuza msitu wa Shakahola kuwa kituo cha kumbukumbu

Tume iliyoundwa na Rais William Ruto kuchunguza vifo hivyo na kupitia kanuni zinazosimamia mashirika ya kidini iliwasilisha ripoti yake mwezi uliopita, ikitaka kuwepo kwa mfumo mchanganyiko wa kujidhibiti sambamba na usimamizi wa serikali.

Ripoti tofauti za Baraza la Seneti la Bunge la Kenya Kenya na shirika la kutetea haki za binadamu linalofadhiliwa na serikali zimesema mamlaka zingeweza kuzuia vifo hivyo.

Juhudi za kudhibiti dini katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi mara nyingi zimepingwa vikali hapo awali kama majaribio ya kudhoofisha uhakikisho wa kikatiba wa mgawanyo kati ya kanisa na serikali.

Nini huwashawishi watu kufuata imani zenye utata za kidini?

02:15

This browser does not support the video element.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW