1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo wa tatu wa Wademocrat wajikita kwenye bima ya afya

13 Septemba 2019

Kwa mara ya kwanza, washindani wakuu wa chama cha Democratic nchini Marekani wanaotaka kuwania urais wameshiriki mdahalo wa pamoja. Joe Biden, Elizabeth Warren na Bernie Sanders ni miongoni mwa wawaniaji 10 waloshiriki.

USA TV-Debatte der demokratischen Präsidentschaftsbewerber
Picha: Getty Images/W. McNamee

Wanawasiasa wanaowania kupeperusha bendera ya chama cha Democrat katika uchaguzi wa rais nchini Marekani mwaka ujao, wameshiriki mdahalo wa tatu usiku wa kuamkia leo. Kwa mara ya kwanza mdahalo huo uliwaleta pamoja washindani wakuu wa chama hicho, waliochuana juu ya masuala muhimu ya kisera ikiwemo kuhusu bima ya afya na mabadiliko ya tabianchi. 

Miongoni mwa wagombea kumi walioshiriki mdahalo huo ulioandaliwa Houston jimbo la Texas, ni pamoja na makamu wa zamani wa rais chini ya utawala wa Barrack Obama Joe Biden, ambaye uchunguzi wa maoni umemweka mbele ya wagombea wengine wote wa chama hicho, pamoja na washindani wake wa karibu Bernie Sanders na Elizabeth Warren.

Tofauti kati ya wazi yadhihirika miongoni mwa wawaniaji

Japo wagombea hao wa chama cha Democratic wameonyesha nia moja ya kumuondoa Rais Trump madarakani, pamoja na haja ya dharura ya kukabili mabadiliko ya tabianchi, tofauti zao zilidhihirika wazi kuhusu suala la megeuzi katika bima ya afya nchini humo.

Seneta Elizabeth Warren akizungumza wakati wa mdahalo wa Wademocrat MarekaniPicha: Reuters/J. Bachmann

Mara kwa mara Joe Biden alikabiliana vikali na washindani wake wakuu kuhusu bima ya afya. Aliwashutumu maseneta Bernie Sanders na Elizabeth Warren kwa kufuatilia ndoto hiyo bila ya mipango ya kuifadhili.

Warren ambaye amekuwa akishangiliwa sana katika kampeni zake kwenye kumbi mbalimbali kando na sera zake za kuwavutia wafuasi wengi, alisema anafahamu kile ambacho kimeharibika na anajua namna ya kukishughulikia na ataongoza kuhakikisha hilo limetekelezwa. Ameongeza kuwa matajiri ndio watagharamia zaidi bima ya afya.

Bima ya Afya yazusha mjadala mkubwa

Naye Sanders anayependekeza kuachana na bima binafsi ya afya ameapa kuhakikisha, hatimaye kila raia wa Marekani atapata huduma ya afya kama haki ya msingi ya binadamu.

Makamu wa zamani wa rais Joe Biden (Kushoto), Seneta wa Massachusetts Elizabeth Warren (Katikati) na Seneta wa California Kamala Harris (Kulia) wakitoa hoja zao wakati wa mdahalo wa WademocratPicha: Getty Images/AFP/R. Beck

Masuala mengine kama uhamiaji, udhibiti wa umiliki wa bunduki, uchumi na hata biashara pia yalijadiliwa huku kila mmoja akijaribu kunadi sera zake na kujitetea dhidi ya ukosoaji.

Kuhusu mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na China, wawaniaji hao waliahidi kuiwajibisha China kutokana na mbinu zake za ufisadi.

Lakini kando na kukosoa vita hivyo vya Trump na China hakuna hata mmoja aliyedokeza kwamba atashughulika kupata suluhisho la haraka akichaguliwa.

Vyanzo: AFPE, RTRE