1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa DFB apendekeza mechi kuchezwa bila mashabiki

20 Aprili 2020

Rais wa shirikisho la kandanda Ujerumani - DFB Fritz Keller amewaomba mashabiki wa kweli kuunga mkono wazo la mechi za Bundesliga kuchezwa bila mashabiki viwanjani ili kuepusha hasara ya kifedha

Deutschland | Coronavirus | DFB Video-Pressekonferenz
Picha: picture-alliance/dpa/GES/M. Gilliar

Akizungumza katika toleo la leo la jarida la michezo la Kicker nchini Ujerumani, Keller amesema na hapa namnukuu "kuifuta michuano ya aina hiyo itamaanisha kuwa "baadhi ya mashabiki huenda wasiweze kuhudhuria mechi ya klabu yao tena kwa sababu klabu hiyo huenda isiwepo tena." Keller amesema hawataki kupoteza klabu yoyote.

Jarida la Kicker hivi karibuni lilisema kuwa vilabu 13 kati ya 36 vya ligi ya daraja la kwanza Bundesliga na ya daraja ya pili huenda vikawa muflisi ifikapo Juni kama malipo ya mwisho ya matangazo ya televisheni hayatalipwa. Na fedha hizo hazitakuwepo kama msimu utafutwa.

Mashabiki wanapinga mechi kuchezwa katika viwanja vitupu kutokana na janga la virusi vya corona kwa sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuhoji kuwa wachezaji wa kandanda hawapaswi kupendelewa ukilinganisha na wengine katika jamii.

Kitengo kinachosimamia ligi hizo mbili za kandanda Ujerumani - DFL kitakuwa na mkutano tena Alhamisi. Vizuizi vya serikali vinaendelea kutekelezwa hadi Mei 3. DFL inatumai kuanza tena mechi na kuukamilisha msimu kuanzia Mei kuendelea mbele na wanasiasa mpaka sasa hawajafutilia mbali kabisa hilo. Lakini mechi bila mashabiki uwanjani zimepigwa marufuku hadi Agosti 31.

Wolfgang Holzhäuser anapendekeza uwekezaji zaidiPicha: picture-alliance/N. Schmidt

Na wakati Keller akigusia suala la vilabu kuangamia, kuna mdau mmoja wa kandanda la Ujerumani anayetoa pendekezo la kuepusha hali kama hiyo katika siku za usoni. Kwamba vilabu vya Bundesliga lazima viwalete wawekezaji zaidi, bila kufuta kanuni maalum ya Ujerumani ya Asilimia 50 jumlisha moja.

Wolfgang Holzhaeuser amechangia katika jarida la leo la michezo Kicker akisema kuwa kawaida kunakuwa na fursa katika migogoro. Na vilabu vya kandanda la kulipwa vinapaswa kuitumia ili kuuweka ufadhili wao kwenye mpango wa muda mrefu, na hivyo kuwa na msingi imara na mpana zaidi. Holzhaeuser aliwahi kuwa mkurugenzi mkuu wa Bayer Leverkusen kwa miaka 24 hadi 2013 na alikuwa na mchango muhimu katika kuanzishwa kwa kitengo cha DFL.

Na sio Ujerumani tu ambapo hali ya kifedha inaleta tumbo joto. Kimbunga cha kifedha kinachoendelea kuvipiga vilabu vya Premier League ya England kutokana na janga la virusi vya corona huenda kikalipiga bara zima katika miezi ijayo wakati kisima cha kufadhili uhamisho wa wachezaji unaogharimu hela nyingi kikikauka.

Kwa misimu minne iliyopita ya usajili, vilabu vya Premier League vimetunisha misuli yao ya kifedha kwa kutumia zaidi ya pauni bilioni moja kwa shughuli za uhamisho wa wachezaji. Hilo limesadia kusambaza utajiri unaotokana na mapato ya mikataba ya televisheni yenye thamani ya mabilioni kote Ulaya

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW