1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUingereza

Mechi za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanza leo

19 Septemba 2023

Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya inaanza hii leo usiku huku mabingwa watetezi Manchester City wakianza kampeni yao dhidi ya Red Star Belgrade ugani Etihad.

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola akibusu Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Inter Milan
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola akibusu Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Inter MilanPicha: Francisco Seco/AP Photo/picture alliance

Manchester City watakaokuwa nyumbani Ettihad watazikosa huduma za majeruhi John Stones, Jack Grealish, Mateo Kovacic na Kevin de Bruyne.

Hata hivyo Erling Haaland, ambaye alikuwa mfungaji bora wa michuano hiyo msimu uliopita, anatarajiwa kuwa kikosini.

John Stones hajacheza tangu mechi ya ngao ya jamii dhidi ya Arsenal huku kiungo Grealish akipata jeraha wakati akiichezea timu yake ya taifa ya England.

Manchester City iliipiga Inter Milan 1-0 mjini Istanbul katika fainali ya msimu uliopita.

Mechi nyengine ambayo inafuatiliwa ni kati ya AC Milan na Newcastle United ugani San Siro.

Newcastle United wamerejea katika michuano hiyo mikubwa ya Ulaya baada ya kukosena kwa miaka 20. Vijana wa Eddie Howe wanakabiliwa na kibarua cha kumenyana na AC Milan, iliyofika nusu fainali msimu uliopita.

Newcastle wanaweza kutiwa moyo kutokana na takwimu inayoonyesha kuwa, klabu hiyo ya Italia imepata ushindi wa mechi moja tu kati ya 11 zilizopita dhidi ya klabu za Uingereza.

Klabu hiyo ya Uingereza ilimsajili kiungo wa zamani wa AC Milan Sandro Tonali aliyejiunga na "Magpies” mwezi Julai.

Huu ni msimu wa 20 wa AC Milan kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa, ikiwa ni idadi ya pili kwa timu za Italia kushiriki michuano hiyo baada ya Juventus (23).

AC Milan ilitolewa kwenye hatua ya makundi mara moja mwaka 2021-22 katika misimu 14 iliyopita.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW