1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUhispania

Arsenal yaishushia mvua ya magoli Barcelona

27 Julai 2023

Washika bunduki wa London Arsenal wanaendelea kujiimarisha kuelekea msimu ujao baada ya kuwafunga mabingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania Barcelona magoli 5-3 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa nchini Marekani.

Premier League | Mikel Arteta
Kocha wa Arsenal Mikel Arteta akitoa maelekezo kwa wachezaji wake wakati wa mchezoPicha: Kirsty Wigglesworth/AP Photo/picture alliance

Timu mbalimbali za Ulaya zinaendelea na michezo ya kirafiki katika kujiandaa kwa msimu mpya.

Mapema leo washika mitutu wa London Arsenal wamewachabanga mabingwa wa Uhispania La Liga Barcelona magoli 5-3 huko Marekani ambako timu hizo zimeweka kambi za kujiandaa kwa mashindano ya  ligi.

Soma zaidiNahodha wa zamani wa Arsenal Granit Xhaka aibukia bundesliga

Kunako dakika ya saba ya mchezo mshambuliaji wa Barcelona Robert Lewandowski aliwatanguliza Barcelona kabla ya Bukayo Saka kusawazisha katika dakika ya 13 ya mchezo, dakika ya 21Arsenal walipata penalti baada ya Araujo beki wa Barca kuunawa mpira katika eneo la ndani ya boksi ingawa Saka aliikosa penalti hiyo.

Mshambuliaji wa Barcelona Robert Lewandoski akishangilia goli licha ya timu yake kupoteza kwa magoli matano kwa matatu mbele ya ArsenalPicha: Emilio Morenatti/dpa/AP/picture alliance

Mpira wa adhabu uliopigwa na Raphael Dias Belloli maarufu Raphinha uliingia kambani na kuitanguliza Barcelona kwa magoli mawili, dakika kumi baadaye sajili mpya ya Arsenal Kai Havertz aliwarudisha Arsenal mchezoni kwa kusawazisha, Leandro Trossard alitupia magoli mawili baaada ya kipindi cha pili kabla ya Fabio Vieira kukamilisha ushindi wa magoli 5-3 dhidi ya vijana wa Xavi.

Kwa upande mwingine Bayern Munich wamechezea kichapo cha magoli mawili kwa moja kutoka kwa Manchester City ya Pep Guardiola huku Real Madrid akiwashushia kipigo mashetani wekundu Manchester United magoli 2-0 na Chelsea wakitoka sare ya goli moja kwa moja na Newcastle united.

Mashabiki wa kandanda nchini Marekani watapata nafasi ya kuishuhudia mechi ya kirafiki ya El-Classico kati ya Barcelona na Real Madrid huko Dallas mnamo siku ya Jumamosi.