1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mechi zaidi zafutwa Premier League ya England

27 Desemba 2021

Wakati aina mpya ya kirusi cha Omicron kikiendelea kusambaa kote England, ligi kuu ya Premier League imefuta mechi kadhaa kutokana na ongezeko la maambukizi, pamoja na wachezaji wengi kujiweka karantini

Premier League Flagge
Picha: Richard Heathcote/empics/picture alliance

Wakati aina mpya ya kirusi cha corona kinachofahamika kama Omicron kikiendelea kusambaa kote Uingereza, ligi kuu ya Premier League ya England imefuta mechi kadhaa kutokana na ongezeko la maambukizi, pamoja na wachezaji wengi kujiweka karantini. Mechi ya kesho kati ya Leeds United na Aston Villa haitaendelea baada ya mechi ya Leeds dhidi ya Liverpool iliyopangwa kuchezwa jana kuahirishwa.

Mpambano wa Wolves na Arsenal pia hautochezwa kesho. Wolves iliomba usogezwe mbele kwa sababu haina idadi ya kutosha ya wachezaji kutokana na Covid na majeruhi. Mechi ya Wolves dhidi ya Watford tayari ilikuwa imeahirishwa jana. Kwa jumla Premier League iliahirisha mechi 15 katika kipindi cha wiki mbili na nusu zilizopita kutokana na visa vya viruso vya corona katika timu mbalimbali.

Suala hili limeibua mjadala wa kuruhusiwa kutumika wachezaji watano wa akiba badala ya watatu kama ilivyo kwa sasa, na makocha wengi wamepaza sauti zao wakiwemo Thomas Tuchel, Patrick Vierra, Ralf Rangnick na wengine wengi. Msikilize Pep Guardiola kocha wa Man City "Lakini tunapozungumza kuhusu maslahi ya wachezaji, hii ndio nchi pekee ambayo haikubali wachezaji watano wa akiba kutumika, ni watatu tu, watatu tu. Kwa nini? Sasa timu zinazocheza zinapaswa kuwalinda wachezaji, tunataka kuwalinda wachezaji kwa kuwatumia wachezaji watano wa akiba. Itakuwa bora zaidi kwa kila mmoja kwa mechi nyingi kama hizi, mwaka baada ya mwaka baada ya mwaka katika mashindano haya, lakini Premier League na vilabu vinasema hapana." Amesema Pep.

Tukiyaweka pembeni hayo ya corona, mabao 28 yalifungwa jana katika burudani la Siku Kuu ya Boxing ijapokuwa hayakubadilisha sana taswira ya vita vya ubingwa. Man City iliibwaga Leicester City 6 – 3 na kujichimbia kileleni na pengo la pointi sita.

Chelsea sasa wametoshana pointi na Liverpool baada ya kutoka nyuma na kuipiku Aston Villa 3 -1. Arsenal wako nyuma yao na pengo la pointi sita baada ya kuwabamiza washika mkia Norwich 5 – 0.

Mahasimu wa Arsenal Tottenham Hotspur wanaongeza shinikizo la nne bora baada ya ushindi wa 3 – 0 dhidi ya Crystal Palace.

AP, AFP, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW