1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meghan aibua ubaguzi Ufalme wa Uingereza

8 Machi 2021

Baada ya mke wa Mwana Mfalme Harry wa Uingereza kuibuwa kashfa kubwa ya ubaguzi wa rangi ndani ya familia ya kifalme, watu kadhaa mashuhuri wamejitokeza kumuunga mkono na kutaka ufalme ubadilishe mtazamo wake.

Meghan und Harry geben Interview bei CBS
Picha: Harpo Productions/Joe Pugliese/REUTERS

Bingwa wa mpira wa tennis duniani, Serena Williams, na mshairi Amanda Gorman wamekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuonesha uungaji mkono wao kwa Meghan Markle, kufuatia tuhuma nzito za ubaguzi wa rangi ndani ya familia ya kifalme ya Uingereza alizozitowa mke huyo wa Mwana Mfalme Harry.

Kwenye mahojiano hayo ya masaa mawili na Oprah Winfrey, Meghan ambaye mama yake ni mweusi, alisema kuwa mumewe Harry alielezea wasiwasi wa familia yake juu ya kiasi gani ngozi ya mtoto wao Archie ingelikuwa nyeusi.

Pia alisema kuwa hakuna hata mtu mwenye kwenye familia hiyo aliyetowa kauli ya kumtetea dhidi ya kuandikwa kibaguzi na magazeti ya udaku nchini Uingereza. Kwa Meghan, mashambulizi hayo yalikuwa sawa na kumtishia maisha yake.

"Nadhani kuna sababu kwamba magazeti haya ya udaku yanakuwa na tafrija zao kwenye kasri la kifalme. Wanaalikwa na kasri lenyewe, kama kwamba kuna mchezo baina yao. Na kwa kuwa tangu mwanzoni mwa uhusiano wetu, walikuwa wakitushambulia na kuchochea chuki nyingi za kibaguzi kiasi cha kwamba mashambulizi hayo yalibadili maisha yetu na kuongeza kitisho, maana haukuwa umbea tu." Alisema mke huyo wa Mwana Mfalme Harry.

Serena, Amanda wamuunga mkono

Meghan Markle akizungumza na Oprah Winfrey kwenye mahojiano maalum.Picha: Joe Pugliese/AP/picture alliance

Mara tu baada ya kutangazwa mahojiano hayo, Serena Williams aliandika kupitia Twitter: "Maneno yake yanaashiria maumivu na ukatili aliokumbana nao. Binafsi najuwa jinsi taasisi za ubaguzi wa kijinsia na rangi pamoja na vyombo vya habari zinavyotumika kutugeuza sisi wanawake na tulio weusi kuwa maadui na kutuvuruga kabisa kabisa."

Meghan alimwambia Oprah kwenye mahojiano hayo yaliyorushwa jana kwamba kuna wakati alishawahi kujaribu kujiuwa baada ya kuingia kwenye familia hiyo ya kifalme na kwamba alikataliwa msaada akiwa kwenye hali hiyo ya matatizo ya kiakili.

Akiandika kupitia Twitter, binti wa mpiganiaji haki za wetu weusi nchini Marekani, Martin Luther King Jr. aitwaye Bernice King, alisema: "Ufalme si ngao dhidi ya fadhaa na majonzi ya ubaguzi wa rangi. Tunaweza kujuwa ubaguzi upo kwenye taasisi na bado tukaumizwa na mtu ambaye ameumizwa nao." 

Mshairi wa Kimarekani mwenye asili ya Afrika, Amanda Gorman, ambaye alipata umashuhuri kwa kughani kwenye sherehe za kuapishwa Rais Joe Biden Januari mwaka huu, amesema familia ya kifalme ya Uingereza imepoteza nafasi ya kubadilika, kwani "Meghan alikuwa fursa pekee ya mabadiliko na muafaka kwenye zama hizi mpya."