1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Meli iliyobeba nafaka yasubiri ukaguzi mjini Istanbul

Sylvia Mwehozi
3 Agosti 2022

Meli ya kwanza iliyobeba shehena ya nafaka kutoka Ukraine tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi mwezi Februari, imewasili jana usiku nchini Uturuki na inasubiri ukaguzi katika mlango bahari wa Bosporus mjini Istanbul.

Türkei Istanbul | Getreide-Schiff Razoni
Picha: Lokman Akkaya/AA/picture alliance

Wizara ya ulinzi ya Uturuki, imesema meli hiyo ya Razoni ambayo iliondoka katika bandari ya Odessa nchini Ukraine siku ya Jumatatu ikiwa na jumla ya tani 26,000 za mahindi kuelekea Lebanon, imetia nanga kwenye mlango bahari wa Bosporus ulioko katika Bahari Nyeusi. Wawakilishi kutoka Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa, watafanya ukaguzi kwenye meli hiyo na baadae kuiruhusu kuendelea na safari kupitia Bahari ya Mediterania.

Mkuu wa timu ya uratibu wa pamoja JCC Ozcan Altunbulak, ameongeza kuwa; ''JCC ina jukumu la kusajili na kufuatilia meli hizo, kupanga na kuwasili kwa meli hizo kwenye bandari za Ukraine, kukagua meli zinazofika na kuondoka Ukraine, kufuatilia masuala ya kiufundi kwa kutumia mawasiliano, zana, sateilaiti na mtandao, kufanya shughuli zote kwa pamoja na pande husika za Ukraine, Urusi na Umoja wa Mataifa.''

Kulingana na takwimu za Ukraine, zaidi ya tani milioni 20 za nafaka kutoka mavuno ya mwaka jana, zinasubiri kusafirishwa. Chakula hicho kinahitajika kwa haraka katika soko la dunia, hususan barani Asia, Afrika na Mashariki ya Kati.Meli ya kwanza yenye nafaka za Ukraine yaondoka Odesa

Chini ya makubaliano ya Julai 22 ya kuondoa vizuizi vya miezi kadhaa vya Urusi dhidi ya bandari, Ukraine iliahidi kuziongoza meli kupitia bahari huku Urusi nayo ikisema kuwa haitoilenga meli yoyote pamoja na miundombinu ya bandari. Waratibu wa makubaliano hayo, Umoja wa Mataifa na Uturuki kwa upande mwingine wamejitolea juu ya usalama na uratibu wa usafirishaji pamoja na kuzifuatilia meli ili kuhakikisha kwamba hazibebi silaha na kuziingiza eneo la vita.

Sehemu ya barabara iliyoharibiwa katika daraja mjini KhersonPicha: Sergei Bobylev/ITAR-TASS/IMAGO

Wakati meli hiyo ya Razoni ikitia nanga, Urusi imeonya kuwa usafirishaji wa meli nyingine utakuwa hatarini endapo nchi za Magharibi hazitokubaliana na "sehemu ya pili" ya makubaliano. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova alisema kuwa wana matarajio nafaka za Moscow, chakula na mbolea pia vitaruhusiwa kuuzwa nje kikamilifu.

Hayo yakijiri, waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema kampeni ya kijeshi ya kuchukua udhibiti kamili wa mkoa wa mashariki wa Donetsk inaendelea kama ilivyopangwa. Kwa upande wake, Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky ametoa wito wa kusaidiwa silaha zaidi kutoka kwa washirika wake akisema Kiev bado haijaweza kuhimili vishindo vya jeshi la Urusi haswa upande wa mizinga na rasilimali watu, katika mapambano ya baadhi ya maeneo ya mkoa wa Donbas.

Jeshi la Ukraine pia limeripoti shambulizi la Urusi katika mkoa wa kaskazini wa Kherson. Kwa wiki kadhaa Kiev imekuwa na matumaini ya kuanzisha mashambalizi ya kushutukiza katika mkoa huo ili kudhibiti tena eneo la kusini.

Naye kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröder ametetea uamuzi wake wa kutojiweka mbali na mshirika wake wa muda mrefu wa kibiashara Vladimir Putin. Schröder amedai kuwa amelaani vita hivyo mara kadhaa lakini kujitenga na Putin hakuwezi kumsaidia mtu yeyote.

Schröder ambaye alikuwa Moscow wiki iliyopita, na kukutana na Putin, ameongeza kuwa "Ikulu ya Urusi, Kremlin inataka suluhisho la mazungumzo" juu ya vita vya Ukraine. Kansela huyo wa zamani amekosolewa kwa miaka mingi juu ya ushiriki wake na makampuni ya umma ya Urusi na usuhuba wake binafsi na Putin.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW