Meli ya gesi ya Urusi yazamishwa
4 Machi 2026
Tukio la kushambuliwa na kuzamishwa kwa meli ya gesiya Urusi katika Bahari ya Mediterenia na mvutano mpya wa kidiplomasia kuhusu nishati na mazungumzo ya amani vimejitokeza.
Kufuatia tukio hilo Urusi imeirushia shutuma Ukraine kwa kushambulia meli yake ya kusafirisha gesi kimiminika, Arctic Metagaz, kwa kutumia droni za majini karibu na pwani ya Libya ambapo taarifa za Urusi zimedai meli hiyo ilizama kufuatia milipuko ya ghafla iliyofuatiwa na moto mkubwa, takribani maili za baharini 130 kaskazini mwa Sirte.
Ugaidi wa kimataifa na uharamia
Taarifa zaidi zinasema wafanyakazi wote 30 waliokuwamo ndani ya meli waliokolewa huku wengine wawili wakipata majeraha ya kuungua ambapo Moscow ilitaja shambulio hilo kama "tendo la ugaidi wa kimataifa na uharamia wa baharini,” ikidai droni hizo zilianzishwa kutoka pwani ya Libya.
Endapo madai hayo yatathibitishwa, itakuwa ni nadra kwa Ukraine kufanikiwa kulenga meli za kivuli za Urusi umbali wa takribani kilomita 2,000 kutoka mipaka yake.
Meli hiyo ilikuwa imewekewa vikwazo na Marekani na Umoja wa Ulaya, na ilikuwa imebeba takribani tani 62,000 za gesi ikielekea bandari ya Port Said, Misri, baada ya kuondoka Murmansk ambapo mpaka sasa Ukraine haijatoa taarifa yeyote ya kukanusha ama kukubali kuhusika na shambulio hilo.
Wakati huo huo, siasa za nishati zimezidi kuwa kitovu cha mvutano barani Ulaya. Rais wa Urusi Vladimir Putin anakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary kujadili usambazaji wa mafuta, huku Hungary na Slovakia zikilalamikia kusitishwa kwa usambazaji kupitia bomba la Druzhba linalopita Ukraine.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliishutumu Kyiv kwa kuzuia kwa makusudi usambazaji huo, akisema wanunuzi wa mafuta ya Urusi wanakabiliwa na usaliti.” Katika sauti yake alisema:
"Unajua kuwa kuna wanunuzi wa mafuta yetu, kama Hungary na Slovakia, ambao kwa sasa wanakabiliwa na usaliti kutoka kwa utawala wa Kyiv. Hii inahusiana na kuzuia kwa makusudi usambazaji kupitia bomba la Druzhba,” alisema Peskov.
Makubaliano kudumu ni Ulaya ishirikishwe
Mjini Washington, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amemtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuongeza shinikizo kwa Moscow na kuhakikisha Ulaya inashirikishwa kikamilifu katika mazungumzo yoyote ya amani.
Merz amesema hakuna makubaliano yatakayodumu ikiwa yatafikiwa bila ushiriki wa Ulaya, na amehoji kama kweli Urusi iko tayari kwa suluhu ya kudumu.
Kwa upande mwingine, shirika la ujasusi la Ujerumani limesema Urusi inaficha gharama halisi za vita, likidai nakisi ya bajeti ya mwaka 2025 ni kubwa zaidi kuliko takwimu rasmi zinavyoonyesha, huku mapato ya mafuta na gesi yakishuka kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi.