Meli ya magari ya kifahari ya Porsche, yatia nanga Kenya
23 Machi 2026
Maelfu ya magari ya kifahari yanayosafirishwa kutoka Japan kuelekea Dubai yameteremshwa kwenye bandari ya kisiwa cha Lamu katika pwani ya Kenya. Mamlaka ya bandari ya Kenya imesema, vita vya Mashariki ya Kati vimeleta faida kwa bandari za Afrika.
Vyombo vya habari vya Kenya vilionyesha magari mengi ya kifahari aina ya Porsche yakiwa yameegeshwa katika ghala moja kwenye bandari hiyo ya kisiwani Lamu, ambacho ni Turathi ya Urithi wa Dunia ya UNESCO. Serikali ya Kenya inakiendeleza kisiwa hicho kwa lengo la kukigeuza kuwa kitovu kingine kikubwa cha usafirishaji.
Kulingana na Meneja wa Bandari hiyo ya Lamu, Abdulaziz Mzee amesema magari hayo yataendelea kubaki bandarini hadi hali itakapotulia na kwamba bandari hiyo inatarajia kupokea meli nyingine ya makontena yenye magari 5,000 wiki ijayo.
Hata hivyo Mzee ameeleza kuwa hili sio jambo la kusherehekea, kwa watu wanateseka lakini amesema wakati huo huo ni baraka ya kibiashara, nchini Kenya.
Bandari ya Jebel Ali Dubai, ilikumbwa na mashambulizi ya anga ya Iran
Magari hayo ya kifahari ni miongoni mwa magari zaidi ya 4,000 ambayo yalilazimika kupakuliwa kisiwani Lamu tangu wiki iliyopita kutoka kwenye meli mbili za kampuni ya Grimaldi Group ya Italia.
Meli ya mwisho yenye shehema ya magari ya kifahari iliondoka kutoka kwenye bandari ya Yokohama nchini Japan mnamo Februari 24, siku nne kabla ya Marekani na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran, vita ambavyo vimesababisha kufungwa kwa safari za meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Bandari ya Jebel Ali huko Dubai ilikumbwa na mashambulizi ya anga ya Iran mnamo Machi mosi. Mamlaka ya Bandari za Kenya imesema kwenye ukurasa wake katika jukwaa la X kwamba Lamu imejiandaa kwa ajili ya ongezeko la kupokea mizigo kutokana na vita vya Iran. Bandari ya Lamu ilitangazwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2012 kama sehemu ya usafiri wa kikanda wa thamani ya dola bilioni 23 inayounganisha Pwani ya Kenya na Sudan Kusini na Ethiopia.
Bandari hiyo ilianza kufanya kazi mwaka wa 2021. Mamlaka ya bandari ya Kenya imesema inatarajia bandari za nchi hiyo kuwa kitovu kinachoongoza cha usafirishaji wa meli barani Afrika.