1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mengi yanatarajiwa kutoka kwa kiongozi mpya wa shirika la biashara duniani, WTO

Josephat Charo1 Septemba 2005

Mengi yanatarajiwa kutoka kwa kiongozi mpya wa shirika la biashara duniani, WTO, Pascal Lamy. Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 58 ni mtu mwenye dima kubwa na ana uwezo mkubwa zaidi akilinganishwa na kiongozi aliyemtangulia. Lamy analifahamu vuzuri shirika hilo la WTO. Mbali na hayo ana mamlaka makubwa na ndio maana mataifa wanachama wa shirika hilo wamemkubali kwa haraka bila mivutano yoyote.

Pascal Lamy, kiongozi mpya wa shirika la biashra duniani, WTO
Pascal Lamy, kiongozi mpya wa shirika la biashra duniani, WTOPicha: AP

Bwana Lamy anakabiliwa na mtihani mkubwa hata kabla ya kazi yake inayomsubiri katika shirika la biashara la dunia, WTO. Mwishoni mwa mwezi Disemba atakutana na mawaziri wa biashara kutoka mataifa wanachama wa shirika hilo mjini Hongkong, ili kujadili juu ya kuyafikia makubalinao ya raundi mpya ya utandawazi katika biashara ya kimataifa.

Raundi hii ya mazungumzo ya Doha, inatuwama juu ya kilimo, soko huru kwa mataifa ya viwanda na huduma. Kwa mtazamo huu kuanzia mwezi Januari mwakani hatua kwa hatua ruzuku, kodi na vikwazo vingine vya kiuchumi vinatakiwa kuwepo. Mazungumzo ya sasa ya Doha yanatakiwa pia kuyazingatia masilahi ya mataifa yaliyoendelea zaidi kiviwanda zaidi duniani katika biashra ya kimataifa.

Kumaliza raundi ya mazungmzo hayo ndilo lengo kubwa la bwana Lamy. Malengo ya pili na tatu ameshayazungumzia tayari wakati alipokuwa akipigania kuchaguliwa kuchukua wadhifa huo. Lakini kuweza kudumisha uchumi ina maana kwamba atakuwa na shughuli nyingi.

Mkutano wa kila mwaka wa shirika hilo mwezi Julai mwaka huu, ulitoa mswada wa kwanza wa maazimio lakini mataifa wanachama wa shirika la WTO hawakukubaliana juu ya rasimu ya maazimio hayo. Sasa Lamy anakabiliwa na kazi ya kuzifufua tena juhudi hizo.

Mwishoni mwa mwezi Julai kamishna wa maswala ya biashara wa umoja wa Ulaya, Peter Mandelson, alisema hatuwezi kuutazama mwezi wa Septemba na matumaini makubwa, ikiwa tutaendelea kushikilia sheria zetu za biashara. Ana matumaini kwamba kiongozi mpya wa shirika la biashara duniani, WTO, atachukua uamuzi wa kibinafsi na kutumia mbinu nyengine ya kutafuta njia itakayolipeleka shirika hilo mbele.

Ni vigumu lakini kusema njia ya sawa ni gani ya kulipeleka mbele shirika hilo. Biashara inakwamishwa na swala tete la kilimo. Ikiwa kilimo ndicho kikwazo kikubwa cha uchumi wa dunia basi kodi inayotozwa bidhaa za kilimo inatakiwa kupunguzwa. Lakini ni vipi kodi hii itakavyopunguzwa? Je kodi itapunguzwa kwa bidhaa ambazo zinahitajika sana au kuweka kipindi maalumu cha kutenda kazi kwa ruzuku kwa bidhaa zinazouzwa katika mataifa ya kigeni? Orodha ya maswali sumbufu ni ndefu na mawazo yanayoweza kutolewa ni mengi.

Mataifa tajiri duniani yanatazamia kuendeleza utajiri wao, kabla kuyashughulikia mataifa mengine. Umoja wa Ulaya na mataifa yaliyoendelea kiviwanda yana mtazamo tofauti. Tayari mataifa hayo yamefanya makubaliano ya kutosha katika maswala ya kilimo, na sasa mataifa hayo pamoja na umoja wa Ulaya, yanataka kusonga mbele na hatua nyengine. Hivyo ndivyo ilivyo katika mzunguko huo, ambapo kila taifa linalikosoa lengine. Maswala yanayosababisha mizozo ni mengi na hata umoja wa Ulaya na Marekani zinazozana juu ya ruzuku kwa wakulina na kodi.

Lamy kama kiongozi mpya wa shirika la biashara duniani,WTO, hana uwezo wa kuyatimiza matarajio ya wengi na kuweza kuondoa vikwazo vya kiuchumi vilivyoko. Anaweza tu kutoa ushauri na kujaribu kutetea maswala fulani yenye umuhimu, lakini hawezi kupitisha maamuzi kwa shirika la WTO. Kwa hiyo maneno aliyoyasema kiongozi aliyemtangulia bwana Lamy, Supachi Panitchpakdi, wakati wa sherehe za kumuaga rasmi hayakuwa ya bure.

Lmy anahitaji uhodari zaidi kuweza kukabiliana na kazi kubwa na kwanza kuweza kuchukua hatua za kwanza zilizo muhimu. Sio uhodari wa kuweza tu kuifanya kazi nyingi iliyopo, lakini uhodari wa kuweza kupitisha maamuzi ya kisiasa ambayo sasa yanatiliwa shaka.

Serikali za mataifa wanachama wa WTO ni lazima zifikirie na kupitisha maamuzi juu ya maswala magumu yanayolikabili shirika hilo, ili yaweze pia kuyapa nafasi maazimo ya mataifa mbalimbali. Mtu kama Lamy anaweza kuyasaidia mataifa hayo, lakini hawezi kuubeba mzigo huo peke yake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW