1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aacha urithi wa mchanganyiko Afrika

2 Desemba 2021

Kansela wa Ujerumani anayeondoka Angela Merkel alijitolea Zaidi kwa ajili ya bara la Afrika kuliko watangulizi wake. Lakini sera zake hazijaonekana kuwa na mabadiliko ya msingi barani humo.

Niger Kanzlerin Merkel auf Afrikareise | Merkel und Präsident Issoufou
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Wakati wa miaka yake 16 akiwa kansela wa Ujerumani, ziara za Angela Merkel barani Afrika ziliongezeka mara kwa mara kama ilivyokuwa mikutano yake na wakuu wa nchi za Afrika. Agosti 2021, Merkel aliwaalika marais kadhaa wa Afrika katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin. Ulikuwa mkutano wa kuaga – na mzuri sana kiasi kwamba Merkel alipata sifa nyingi kutoka Afrika. Minehle Nene, mtafiti katika Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Afrika Kusini – SAIIA anasema ushirikiano wa Merkel na Afrika umekuwa mzuri hasa kuhusiana na maendeleo ya kiuchumi barani humo. "Amefanya kazi nzuri sana ya kuiweka Afrika katikati ya sera ya kigeni ya Ujerumani na ajenda ya maendeleo na kuendelea kwake kujitolea kuikuza Afrika katika siasa za Ujerumani kulidhihirika wazi hata katika maingiliano yake na viongozi wa Afrika na kuhusika kwake katika bara hilo." Amesema Nene. Nene ameiambia DW kuwa uwekezaji wa Ujerumani Afrika umepanuka kiasi katika miaka ya karibuni chini ya uongozi wake.

Viongozi wa Afrika wausifia mpango wa Compact with Africa wakati wa mkutano wa BerlinPicha: Michele Tantussi/REUTERS

Nia ya kweli barani Afrika

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Akinwumi Adesina, pia amemwagia sifa kansela huyo wa Ujerumani anayeondoka. Kwenye Makala aliyoandika kwenye tovuti ya DW, Adesina alisema Merkel amekuwa Rafiki wa karibu na wa kweli kwa Afrika.

Adesina anasifu hasa wazo la G20 Compact Afrika, ambalo lilizinduliwa chini ya mpango wa Merkel katika mwaka wa 2017 wakati Ujerumani ilikuwa rais wa G20. Chini ya mpango huo, kuna ushirikiano kati ya mataifa ya G20, ikiwemo Ujerumani na nchi 12 za Kiafrika.

Soma pia: Kansela Angela Merkel ahimiza uwekezaji barani Afrika

Kampuni ya VW ina kiwanda cha magari KigaliPicha: picture-alliance/Photoshot

Mtalaamu Minenhle Nene pia anauona mpango wa Compact with Africa kuwa wa mafanikio. Anasema makampuni mengi ya Ujerumani yamekuwa yakisita kuwekeza Afrika. Lakini sasa yanajihusisha Zaidi barani humo, sehemu kubwa ikiwa ni kutokana na mpango huu.

Uwepo mdogo wa Ujerumani

Nene anaonya hata hivyo, kuwa mpango huo unahitaji muda ili uwe imara. Anasema hatupaswi kutarajia mabadiliko kutokea mara moja, akiongeza kuwa mpango wa Compact with Africa unalenga kujenga mahusiano ya muda mrefu na yakuzifaidi pande zote.

Afrika kwa sasa inachangia asilimia moja pekee ya uwekezaji wa Ujerumani ulimwenguni. Zaidi ya hayo, karibu makampuni 800 pekee yamewekeza barani humo. Kwa sababu hizo, mchambuzi Gerrit Kurtz kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Sera ya Umma mjini Berlin, anaukosoa mpango huo wa Merkel. "Mpango wa Compact with Africa haukutimza lengo lake la kukuza uwekezaji wa sekta binafsi ya Ujerumani barani Afrika na haukufikia matarajio yake, yakiwemo yale yaliyochochewa na Kansela mwenyewe." Anasema Kurtz.

Ziara za Merkel Afrika ziliongezeka wakati muhula wake ukikaribia ukingoniPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Ushirikiano wa mageuzi

Kurtz pia anakosoa kile kinachofahamika kama "ubia wa mageuzi” wa sera ya ushirikiano wa maendeleo ya Ujerumani. Chini ya ushirikiano huu, nchi za Afrika hupokea misaada ya ziada kama serikali ya Ujerumani inaziona kuwa zinapiga hatua Fulani katika utawala bora.

Ethiopia, kwa mfano, imekuwa mshirika wa mageuzi tangu 2019. Hivi karibuni, nchi hiyo imekumbwa na ukosoaji wa kimataifa kwa sababu ya vita vinavyoendelea katika mkoa wake wa kaskazini wa Tigray.

Licha ya mapungufu hayo, Kurtz anaamini Angela Merkel alisaidia kuongeza umuhimu wa Afrika kwa sera ya kigeni ya Ujerumani. Anahisi serikali za awali ziliichukilia Afrika kuwa suala la maendeleo, ambapo Merkel alitanua hilo kujumuisha mtizamo wa kiuchumi.

Hata hivyo, Kurtz anaamini kuna maslahi ya wazi ya kibinafsi nyuma ya Ujerumani kujihusisha Zaidi na Afrika.

Jeshi la Ujerumani katika eneo la SahelPicha: DW/F. Muvunyi

Idadi ya ziara za Merkel barani Afrika ziliongezeka mwaka wa 2016, mwaka mmoja baada ya kile kilichofahamika kama mzozo wa uhamiaji wa Ujerumani wakati wahamiaji milioni moja na waomba hifadhi waliwasili nchini.

Anasema wasiwasi wa Merkel katika kupunguza uhamiaji usio wa kawaida barani Ulaya, ambao ulikuwa kipaumbele cha washirika wa Ujerumani katika Umoja wa Ulaya, hasa Ufaransa, uliathiri baadhi ya sera nyingine za Ujerumani Afrika.

Msaada wa Merkel Afrika Magharibi

Wakati wa uongozi wa Merkel, maslahi ya Ujerumani yamehama kutoka Afrika Mashariki hadi Afrika Magharibi, Merkel aliiambia DW katika mahojiano. Ujerumani imetanua pakubwa ushirikiano na mataifa ya Sahel ya Mali, Mauritania, Chad, Burkina Faso na Niger.

Soma pia: Rais wa Ghana asisitiza uwekezaji zaidi barani Afrika

Eneo la Sahel limeshuhudia ukosefu wa usalama katika miaka ya karibuni, huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo wa itikadi kali na makundi ya uasi. Bado haijulikani Afrika itakuwa na umuhimu kiasi gani kwa mrithi mtarajiwa wa Merkel Olaf Scholz. Makubaliano ya serikali ya muungano ya vyama vitatu vya SPD, Kijani na FDP, hayajalitaja bara hilo. Lakini mtalaamu Kurtz anatumai kuwa Ujerumani itaendelea kujitolea barani Afrika.

Makala hii imetafsiriwa kutoka kwa Kijerumani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW