1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Merkel na Seehorfer haujatatuliwa

17 Juni 2018

Kansela Angela Merkel anapambana kuuepusha mgogoro ndani ya muungano wake kuhusiana na sera ya wakimbizi akijaribu kuandaa mkutano wa nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya kabla ya mkutano wa viongozi wote wa EU

Deutschland 2015 Bundespressekonferenz | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Kansela Angela Merkel anapambana kuuepusha mgogoro ndani ya muungano wake kuhusiana na sera ya wakimbizi akijaribu kuandaa mkutano wa nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya kujadili suala hilo kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wote wa Umoja huo utakaofanyika Juni 28 mpaka 29. Hayo yameripotiwa Jumapili 17.06.2018 na gazeti moja la Ujerumani.

Gazeti la Bild limenukuu duru za serikali kutoka Umoja wa Ulaya ambapo limeandika kwamba kansela Merkel anataka kuzungumzia uwezekano wa kutafuta suluhisho na Ugiriki,Itali na Austria. Gazeti hilo limeongeza kumnukuu mjumbe wa serikali ya Itali katika Umoja huo wa Ulaya akisema kwamba bado hawajafikia makubaliano na kwamba hivi sasa wako katika awamu ya maandalizi. Pia haijawa wazi haswa ni lini mkutano huo maalum wa kilele utafanyika.

Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Msemaji wa serikali ya Ujerumani hakuweza kupatikana mara moja kutoa tamko juu ya ripoti hii. Nchi za Umoja wa Ulaya zimegawika kwa kiasi kikubwa kuhusu jinsi ya kushughulikia idadi kubwa ya watu wanaokimbia migogoro na hasa kutoka Mashariki ya Kati.  Suala hili limeonekana wazi kuongezeka katika kipindi cha wiki iliyopita ambapo serikali ya Itali ilikataa kuiruhusu meli iliyosheheni mamia ya wahamiaji kufunga katika bandari yake.

Merkel anashikilia msimamo kwamba sera ya wakimbizi inaweza tu kukubaliwa kwa mafanikio na kutekelezwa katika ngazi ya Umoja wa Ulaya na msimamo huu umemuweka katika mgongano na washirika wa chama chake mwenyewe kutoka Bavaria pamoja na waziri wake wa mambo ya ndani anayetaka Ujerumani ichukue uamuzi wa kivyake kushughulikia suala la wakimbizi.

Wabavaria wametishia kumkiuka  Merkel na Jumatatu wakaendelea na mipango ya  ambayo Merkel aliamua kuizuia.Pendekezo la waziri wa mambo ya ndani Horst Seehorfer ni kwamba Ujerumani itawarudisha wanakotoka wahamiaji ambao tayari wameshajisajili katika nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Kimsingi mpango huu utahujumu mamlaka ya Merkel ambayo inasimamia mwelekeo wa kuacha milango wazi kwa wakimbizi tangu mwaka 2015. Mpango wa Seehorfer unakwenda kinyume kabisa na anachokisimamia Merkel na pia utakuwa ni pigo kubwa kwa utaratibu wa Umoja wa Ulaya wa kuacha wazi mipaka yao katika mfumo wa pamoja unaojulikana kama Schengen. Waziri wa mambo ya ndani anasisitiza kwamba chama chake cha Christian Social Union hakina dhamira ya kumporomosha Merkel na serikali yake  ingawa hakuna dalili bado ya kufikiwa mwafaka katika mgogoro huu.

Picha: Imago/Ipon

Kansela Merkel amewaomba washirika wa chama chake kutoka Bavaria CSU kumpa muda wa wiki mbili kutafuta mipango ya pamoja na nchi kama Itali na Ugiriki kama ule uliofikiwa kati ya  Uturuki na Umoja wa Ulaya mnamo 2016. Kwa mujibu wa gazeti la Bild haijabainika ikiwa Uhispania na nchi nyingine kutoka eneo la Balkan zitashiriki katika mkutano wa Merkel.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Sylvia Mwehozi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW