Merkel aelekea Algeria kulijadili suala la uhamiaji
17 Septemba 2018Lengo kuu la ziara ya Merkel nchini Algeria ni kuimarisha mahusiano ya kibiashara, ambapo Shirika la habari la Algeria limesema itatoa fursa ya kutathmini hatua zilizopigwa katika mahusiano ya kiuchumi kati ya Algeria na Ujerumani na jinsi ya kuyaimarisha.
Lakini mazungumzo ya Merkel na Rais Abdelaziz Bouteflika na Waziri Mkuu Ahmed Ouyahia yanatarajiwa kulenga pia uhamiaji. Algeria ndio nchi kubwa kabisa katika kanda hiyo, ikipakana na Mali na Niger katika upande wa kusini.
Wahamiaji wengi husafiri kupitia nchi hizi ili kufika katika bahari ya Mediterania na kujaribu kuingia Ulaya
Hapo jana, Kansela Merkel na mwenzake wa Austria Sebastian Kurz walionekana kuweka kando tofauti zao, wakati viongozi hao wawili walipotangaza msururu wa hatua zinazolenga kupambana na uhamiaji haramu barani Ulaya. Merkel na Kurz walikubaliana katika mkutano wao wa jana mjini Berlin, kushirikiana na mataifa kadhaa ya Afrika ili kuzuia mmiminiko wa wahamiaji na wakaikaribisha mipango ya Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker ya kuiongeza idadi ya wafanyakazi wa ulinzi wa mpakani hadi 10,000 ifikapo mwaka wa 2020.
Ijapokuwa Merkel na Kurz awali walitofautiana kuhusu uhamiaji, kansela wa Austria anayepinga uhamiaji alikiri kuwa Ujerumani imechukua msimamo imara, kwa sehemu kubwa kutokana na Waziri wa Mambo ya Ndani Horst Seehofer.
Na wakati Merkel akielekea Afrika, Kurz atakuwa na mazungumzo na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Paris leo kabla ya mkutano wa wiki ijayo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Salzburg.
Kansela huyo wa Austria amesema mwezi Desemba ataandaa mkutano wa kilele mjini Vienna kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika pamoja na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, ili kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na bara hilo katika juhudi za kudhibiti uhamiaji.
Wakati huo huo, zaidi ya watu 1,000 waliandamana kupinga sera ya uhamiaji ya Ujerumani katika mji wa mashariki wa Koethen, wakiwa wamezingirwa na karibu polisi 500 wa kuzuia ghasia. Walibeba mabango yaliyomtaka Kansela Merkel kujiuzulu.
Kwingineko, zaidi ya watu 12,000 waliandamana jana dhidi ya ubaguzi wa rangi kote magharibi mwa Ujerumani. Ni wiki mbili baada ya kutokea vurugu za watu wa mrengo mkali wa kulia katika upande wa mashariki mwa Ujerumani. Waandamanaji walimiminika katika mitaa ya miji ya Cologne, Dortmund na Gelsenkirchen kuitaka serikali ya Ujerumani kusitisha kuwarudisha watu katika nchi kama vile Iraq na Aghanistan.
Wapinzani wa sera hiyo wanasema mataifa yote mawili ni hatari kwa watu kurejeshwa nyumbani na badala yake wanapaswa kuruhusiwa kuishi Ujerumani.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel
https://www.dw.com/en/germanys-angela-merkel-backs-austria-on-stronger-eu-borders/a-45513221
https://www.dw.com/en/merkel-in-algeria-migration-likely-to-influence-trade-talks/a-45501791