1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aelezea matumaini ya kumaliza mkwamo wa kisiasa

7 Januari 2018

Kansela Angela Merkel ameelezea matumaini wakati akianzisha mazungumzo na chama cha pili kwa ukubwa nchini Ujerumani ya kuunda serikali ya muungano

Deutschland Sondierungsgespräche in Berlin Merkel und Schulz
Picha: Reuters/H. Hanschke

Mikutano inayoanza kati ya Merkel na vyama ndugu vya kihafidhina vya Merkel – CDU na CSU na kile cha Social Democtratic – SPD itatathmini kama pande zote zina msimamo wa pamoja wa kuwezesha kuanzishwa mazungumzo rasmi ya kuundwa serikali mpya ifikapo Machi au Aprili mwaka huu.

"nnaingia katika mazungumzo haya na matumaini. Wakati huo huo, ni wazi kwangu kuwa kuna kiasi kikubwa cha kazi iliyopo mbele yetu katika wiki chache zijazo, lakini tuna dhamira ya kuikabili hali hiyo ili kupata matokeo mazuri". Merkel aliwaambia wanahabari wakati akiwasili katika makao makuu ya SPD kwa ajili ya mkutano huo.

Kiongozi wa CSU Horst SeehoferPicha: Reuters/H. Hanschke

Mazungumzo hayo yana vizingiti kadhaa, ikiwa ni pamoja masuali magumu yanayohusiana na zaidi ya waomba hifadhi zaidi ya milioni moja ambao wamewasili Ujerumani tangu mwaka wa 2015. Kiongozi wa CSU Horst Seehofer ameelezea matumaini ya kupatikana muafaka na SPD.

Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz wakati huo huo ameashiria kuwa chama chake kinakwenda katika mazungumzo hayo kiwa na mawazo ya wazi, wakati kikiwa kimedhamiria kutafuta maelewano kuhusu mageuzi kuhusu masuala ya ustawi wa jamii.

Wakati pande zote zikikabiliana kwenye meza ya mazungumzo, vyama hivyo vimekubaliana kukataa mahojiano yoyote katika vyombo vya habari, huku yatakayozungumzwa yakitakiwa tu kutolewa kupitia taarifa za pamoja.

Uamuzi huo unalenga kuepusha marudio ya juhudi za awali zilizoshindwa za Merkel katika kuunda serikali ya muungano mwaka jana, wakati mahojiano yaliyofanywa na wajumbe yalichafua mazingira yaliyokuwapo.

Uchunguzi wa maoni wa karibu hata hivyo unonyesha kuwa ni wajerumani wachache wanaounga mkono kuundwa kwa serikali ya muungano.

Uchunguzi uliochapishwa na jarida la Focus lilipata kuwa asilimia 34 ya Wajerumani wanapendelea uchaguzi mpya, wakati asilimia 30 pekee wanaunga mkono kurejeshwa muungano wa vyama vya kihafidhina CSU/CSU na SPD.

Uchunguzi mwingine uliochapishwa na shirika la habari la umma la ARD ulipata kuwa asilimia 45 ya Wajerumani wanauchukulia kwa uzuri muungano mpya wa serikali, wakati asilimia 52 wakisema utakuwa kitu kibaya.

Mwandishi: Bruce Amani/DPAE
Mhariri: Zainab Aziz

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW