Merkel aionya Urusi kuhusu vikwazo vipya
5 Machi 2015Mzozo nchini Ukraine, hali nchini Ugiriki na mkataba wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani ni mada zilizopewa kipaumbele katika mazungumzo kati ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jean Claude Juncker mjini Brussels.
Merkel amewaambia waandishi wa habari kwamba jukumu lililopo sasa ni kuzuia umwagaji damu mashariki ya Ukraine, ambako mkataba dhaifu wa kusitisha mapigano unaonekana kuheshimiwa licha ya visa vya ukiukaji, tangu uliposainiwa Februari 12 mwaka huu katika mji mkuu wa Belarus, Minsk. "Kwa sasa tuna mkataba dhaifu wa usitishaji mapigano unaohitaji kuimarishwa. Ni dhahiri kwamba ikiwa mkataba wa Minsk utakiukwa kwa kiwango kikubwa, baraza la Ulaya na halmashauri ya Umoja wa Ulaya ziko tayari kuandaa na kuweka vikwazo zaidi."
Ukraine ilisema jana kwamba waasi wanaoiunga mkono Urusi wanaendelea kuukiuka mkataba wa kusitisha mapigano kwa kuwashambulia wanajeshi wa serikali. Baraza la usalama la kitaifa mjini Kiev limesema mwanajeshi mmoja ameuwawa na mwingine kujeruhiwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Merkel alisema wamezungumzia kuhusu umuhimu wa kurejesha dhima ya uhuru wa Ukraine na kuhakikisha inayadhibiti tena maeneo yake yaliyo mikononi mwa waasi. "Heshima ya mpaka inaweza kurejeshwa iwapo kutakuwa na maafisa wa Ukraine katika mpaka wa Urusi," aliongeza kusema Merkel.
Akizungumza baada ya kikao cha jana Jean Claude Juncker alifutilia mbali mipango yoyote ya kufanya mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi katika siku zijazo. "Tumejadiliana kwa kina kuhusu mzozo wa Ukraine na athari zake nchini humo. Tumezungumzia pia mkataba huru wa kibiashara kwa sababu baadhi ya makamishna wanaohusika na suala hilo wamefaulu kuujadili pamoja nasi."
Mkataba wa kibiashara na Marekani uafikiwe mwaka huu
Mada nyingine zilizokuwa katika ajenda ya mazungumzo kati ya Merkel na Juncker ni juhudi za kuimarisha ukuaji uchumi, kutengeneza nafasi za ajira barani Ulaya na mkataba mkubwa kabisa wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.
Kansela Merkel ameuunga mkono mkataba huo licha ya ukosoaji kutoka kwa makundi ya watumiaji bidhaa yanahofia kushuka kwa ubora wa viwango na kupotea kwa udhibiti kutokana na mfumo wa kusuluhisha mivutano ya uwekezaji wenye utata.
Merkel amesema Ujerumani na halmshauri ya Ulaya zinataka mkataba wa kibiashara uafikiwe mwaka huu. "Tunataka kuisaidia kamisheni ya Ulaya kulifikia lengo hili. Ikizingatiwa kasi ya mazungumzo nadhani ni muhimu kwa nafasi za ajira hapa Ulaya tusonge mbele haraka kuupata mkataba. Lakini bila shaka tuna viwango vyetu Ulaya na tunahitaji kuvizingatia. Hiyo ni sehemu ya kazi yetu na ni suala tunalohitaji kulikariri kila siku."
Mkataba wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani umekuwa ukisuasua kwa zaidi ya mwaka mmoja huku pande zote mbili zikijaribu kutafuta makubaliano kuhusu kila kitu kuanzia sekta ya huduma za fedha hadi usalama wa chakula.
Merkel na Juncker wameonya dhidi ya kubashiri kwamba Ugiriki itahitaji msaada wa tatu wa fedha kuisaidia kuondokana na mzigo wake wa madeni.
Mwandishi: Josephat Charo/AFP/DPA/REUTERS
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman