1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aishauri Japan kukabiliana na madhila ya vita

Admin.WagnerD9 Machi 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Ujerumani iliweza kurejea katika nafasi ya hadhi katika jamii ya kimataifa kwasababu ya juhudi zake za kukabiliana na madhila iliyofanya wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia

Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Merkel ameikumbusha Japan ya kuwepo haja ya kukabiliana na historia yake ya zamani kuhusu vita lakini amezitaka pia nchi jirani na Japan kutekeleza wajibu wao ili kufikia maridhiano.

Matamshi ya Merkel aliye katika ziara ya siku mbili nchini Japan yanakuja huku Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe akijiandaa kutoa taarifa ya kuadhimisha miaka sabini tangu kukamilika kwa vita vikuu vya pili vya dunia, historia ambayo mpaka sasa inatatiza uhusiano kati ya Japan, China na Korea Kusini.

Taarifa hiyo itafuatiliwa kwa karibu na China na Korea Kusini ambao waliathirika pakubwa chini ya ubabe wa kijeshi wa Japan na hata Marekani itataka kujua msimamo na mtizamo wa Japan kuhusu kujaribu kuyashughulikia madhila ya kipindi cha nyuma.

Je Japan itaomba msamaha?

Abe amesema katika kipindi cha nyuma kuwa ananuia kuelezea masikitiko yake kuhusu vita hivyo na baraza lake la mawaziri linazingatia radhi zilizotolewa kipindi cha nyuma ikiwemo tamko muhimu lililotolewa na waziri mkuu wa zamani wa Japan Tomiichi Murayama mwaka 1995. Hata hivyo haijabainika wazi kama Abe binafsi ataomba msamaha kwa madhila ya kipindi hicho cha vita vikuu au la.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo AbePicha: Getty Images

Katika hotuba yake ya mwanzo wa ziara yake inayoanza leo nchini Japan tangu alipozuru mara ya mwisho mwaka 2008, Merkel amenukuu hotuba iliyotolewa na Rais wa zamani wa Ujerumani marehemu Richard von Weizsaecker ambayo alisema kukamilika kwa vita vikuu vya pili vya dunia barani Ulaya ilikuwa siku ya ukombozi na kuongeza wale wanaofumbia macho historia yao ni vipofu wa nyakati za sasa.

Japan ijifunze kutoka kwa Ujerumani

Merkel ameitaka Japan kujifunza kutoka kwa Ujerumani jinsi ilivyojikwamua kutoka kwa sifa mbaya ya kuhusishwa na madhila, mateso na ukatili wa vita na kuamua kutafuta maridhiano na msamaha na majirani zake na ulimwengu kwa jumla kwa kukabiliana na hali halisi ya mambo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini TokyoPicha: Reuters/K. Sasahara

Kansela huyo wa Ujerumani hata hivyo amesema ni vigumu kwake kuishauri Japan jinsi ya kujiendesha na majirani zake

Uhusiano kati ya Japan na majirani zake China na Korea Kusini umedorora hata zaidi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na migogoro ya mipaka. Chini ya utawala wa Abe, Japan inaonekana kuimarisha mbinu za kuficha makosa ya nyakati za vita.

Merkel atakutana na mfalme mkuu wa Japan Akihito katika kasri lake kabla ya kufanya mkutano rasmi na Abe ambapo masuala kadha wa kadha ukiwemo mzozo wa Ukraine yanatarajiwa kujadiliwa.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Ap/Afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman