Merkel aisifu Jordan kwa kuwahifadhi wakimbizi wa Syria
21 Juni 2018Vitendo vya uchokozi vya Iran sio tu vinahitaji kujadiliwa, lakini tunahitaji suluhisho la haraka," alisema kansela Merkel baada ya kukutana na mfalme wa Jordan Abdullah mjini Amman.
Ujerumani itaendelea kuwa sehemu ya makubaliano ya kinyuklia na Iran, ambayo yaliondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo kwa kubadilishana na udhibiti wa mpango wake wa kinyuklia, baada rais wa Marekani Donald Trump kujiondoa kutoka mkataba huo mwezi Mei mwaka huu.
Merkel alisema kwamba wakati nchi za mataifa ya Ulaya yanataka kuendelea na makubaliano hayo yaliyfikiwa mwaka 2015, mataifa hayo yana wasi wasi kuhusu mpango wa makombora wa Iran, kuwapo kwake nchini Syria na jukumu lake katika vita nchini Yemen.
Kansela Merkel aliwasili nchini Jordan kama sehemu ya ziara yake ya siku mbili ambayo pia itamfikisha nchini Lebanon , nchi mbili ambazo zimeathirika mno na mzozo unaoendelea nchini Syria.
Merkel aipongeza Jordan
Pia ameipongeza Jordan kwa kuwapokea wakimbizi wa Syria. Nchi hiyo ya kifalme imewapokea wakimbizi karibu 650,000 kutoka Syria. Kuhusu sera ya kufungua milango kwa wakimbizi nchini Ujerumani, kansela amesema mazungumzo yanaendelea kuhusu sea bora zaidi, lakini hakuna shaka ya kufunga milango.
"Nadhani kwa kiasi kikubwa hakuna haja ya kuwa na hofu , na bila shaka naweza kusema hakuna mtu anayeweza kufunga mipaka. Na kwa kiasi kikubwa Ujerumani ni salama, licha ya kuwa kunatokea matukio ambayo shutuma hutupwa kwa wageni kwa mashambulizi. Lakini pia kuna wakati wakimbizi hasa wanawake wameuwawa. Kwa hiyo shutuma zinakwenda kwa pande zote."
Kansela ameahidi mkopo wa dola milioni 100 kwa Jordan , ambako maandamano ya hivi karibuni yamelazimisha baraza la mawaziri kujiuzulu mwezi huu kuhusiana na hatua za kubana matumizi. Merkel amesema mkopo huo, ambao unakuja baada ya mkopo mwingine wa euro milini 384 ambao Ujerumani uliiahidi Jordan mwaka huu, una lenga kusaidia juhudi za nchi hiyo kutekeleza mageuzi ambayo yanatakiwa na shirika la fedha la kimataifa.
mapema leo, Merkel alihutubia wanafunzi katika chuo kikuu cha Ujerumani na Jordan mjini Amman , chuo kikuu cha tatu kikubwa nchini Jordan, ambacho kilianzishwa mwaka 2005. Kiasi ya Wajerumani 100 wanashirika katika kukiendesha chuo hicho na kuandika mitaala ya chuo pamoja na ziara ya masomo nchini Ujerumani na Austria. Merkel pia atakutana na wanajeshi wa Ujerumani walioko Jordan kama sehemu ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kupambana na wanamgambo wa kile kinachojulikana kama Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga