1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aitaka China kuzungumzia haki za binaadamu

28 Aprili 2021

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ametoa wito wa kuanza tena mazungumzo ya haki za binaadamu na China, huku Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang akikiri kuwepo tofauti ya mtazamo katika uhusiano kati ya Ujerumani na China.

Deutschland Angela Merkel China  Premierrminister Li Keqiang
Picha: MICHELE TANTUSSI/REUTERS

Akizungumza siku ya Jumanne na Keqiang katika mashauriano yake ya mwisho ya kiserikali na China kama kiongozi wa Ujerumani, Merkel amerudia kuelezea umuhimu wa kuanza tena haraka iwezekanavyo mazungumzo kuhusu haki za binaadamu pamoja na uhusiano wa kidplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Katika mkutano baina ya viongozi hao wawili uliofanyika kwa njia ya video, Merkel amesema mazungumzo hayo ya kawaida yameimarisha ushirikiano katika masuala kuanzia mabadiliko ya hali ya hewa hadi kwenye biashara na wakati mwingine yamegusia maeneo mengine magumu wasiyokubaliana pamoja kama vile haki za binaadamu na Hong Kong.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi na mwenzake wa Ujerumani, Heiko Maas Picha: Reuters/M. Sohn

"Katika muktadha huu, mada ya haki za binaadamu kijadi ina jukumu kubwa katika mazungumzo yetu ya mara kwa mara. Kuna maoni tofauti hapa, hasa tunapoifikiria hali ya Hong Kong, kwa mfano. Hadi sasa tumefanikiwa kuyashughulikia masuala haya vizuri na ninatumai kwamba tunaweza kufanikisha mazungumzo ya haki za binadamu haraka iwezekanavyo," alisisitiza Merkel.

Merkel amesema mizozo inaweza ikatatuliwa tu kwa kufanya mazungumzo. Ameongeza kusema kuwa ana matumaini kwamba mazungumzo kati ya serikali hizi mbili yataendelea hata baada ya yeye kuondoka madarakani.

Katika mkutano huo uliowashirikisha pia mawaziri wengine wa serikali, Waziri Mkuu wa China Li Keqiang amekiri kuwepo tofauti ya mtazamo katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili, ingawa hakugusia haki za binadamu.

Ushirikiano ni muhimu

Li amesema China na Ujerumani zinapaswa kuonyesha ushirikiano na umoja katika harakati zao za kuufufua uchumi wa ulimwengu.

Familia za wafanyabiashara wa Kijerumani wanaofanya kazi ChinaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Probst

Wizara ya mambo ya nje ya China imesema katika taarifa yake kwamba ikiwa nchi hizo mbili zitaheshimu maslahi muhimu ya kila mmoja na zinawasiliana kwa misingi sawa na kutoingiliana katika masuala yao ya ndani, zinaweza kuanzisha mazingira mazuri kwa kuendeleza ushirikiano imara.

Kansela Merkel pia ameitaka China kushiriki na kuonyesha uwazi katika mazungumzo ya pamoja ya kuidhinisha na kutengeneza chanjo ya virusi vya corona, hasa na Shirika la Afya Duniani, WHO. Merkel amesema janga la COVID-19 litaweza kudhibitiwa kwa ushirikiano wa pamoja.

Wakati wa mazungumzo hayo, Joe Kaeser, mwenyekiti wa kamati ya mataifa ya nchi za Asia na Pasifiki anayehusika na Biashara ya Ujerumani amekariri wasiwasi wa kampuni za Ujerumani kuhusu mahitaji ya kuhifadhi data za ndani nchini China na vizuizi juu ya uhamasishaji wa data za kuvuka mipaka.

Kaeser amesema China imekuwa ikizuia kutolewa taarifa kwa uwazi katika manunuzi kwenye kampuni zinazomilikiwa na serikali.

(DPA, Reuters)