1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ajitolea kupambana na mabadiliko ya tabianchi

31 Desemba 2019

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ametumia ujumbe wake wa Mwaka Mpya kuahidi kwamba jitihada zote za kibinaadamu zitatumika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Angela Merkel Neujahrsansprache SPERRFRIST
Picha: Reuters/M. Tantussi

Wapenzi wananchi wenzangu,

Leo sio tu tuko mwanzoni mwa mwaka mpya, bali pia muongo mpya. "Ninashawishika kuamini kuwa tuna sababu nzuri za kuwa na imani na miaka ya 20 ya karne ya 21 itakuwa mema, endapo tutatumia nguvu zetu, ikiwa tutagemea kile kinachotufanya tuwepo kuunganisha nguvu zetu tunapokumbuka yale ambayo kwa pamoja tumeyafanikisha kwenye miongo hii michache.

Mwakani, Ujerumani itakuwa imeungana tena kwenye amani na uhuru kwa miaka 30 sasa. Tumefanikisha mambo mengi makubwa kwenye miaka hii 30. Kwa mfano, hapajawahipo kuwapo na wengi wenye ajira kama kipindi hiki. Hata hivyo, bado kuna mengi ya kufanywa wakati tunapofikiria miaka 30 iliyopita. Wakati huo huo, tumeshuhudia kila siku namna maendeleo ya kidijitali yanavyoyabadili maisha yetu kwenye maeneo yote, na hapana shaka ajira zetu. Tunapaswa kupata majibu mapya kwa changamoto hii. Kwa sababu tunataka kila mmoja kuwa na fursa ya kupata elimu inayohitajika kwa mabadiliko haya. Tunataka watu wawe na uhakika na usalama wa ajira huko tuendako pia, na pensheni ya kuaminika wakifikia uzeni."

Ili kulifanikisha hayo, ni lazima tuwe na ujasiri wa kufikiria upya na tuwe na nguvu za kuachana na njia kongwe za mazowea, na tuwe na utayari wa kujaribu mambo mapya, na moyo wa kutenda haraka, tukiamini kwamba hata yale yasiyo ya kawaida yanaweza kufanikiwa ili kizazi cha sasa na watoto wao waweze bado kuishi kwenye sayari hii ya dunia.

Kupanda kwa joto katika sayari yetu ya dunia kunatisha. Hili ni miongoni mwa mambo yanayotengenezwa na binaadamu wenyewe. Kwa hivyo, tunapaswa kufanya kila liwezekanalo kibinaadamu kukabiliana na changamoto hii. Bado inawezekana. Mpango wa ulinzi wa mazingira ambao serikali kuu ya shirikisho umeupitisha siku chache zilizopita unachukuwa jukumu hili. Nafahamu vyema kwamba hatua zilizopitishwa zinawafanya wengine wahofie kwamba zitawalemea sana na kwa wengine wanaona hazitoshi kabisa.

Na hili ni la kweli pia: mimi nina miaka 65 sasa, kwenye umri ambao binafsi pengine sitaona matukio yatakayojiri endapo tulio kwenye siasa hatutachukuwa hatua sasa. Ni watoto na wajukuu zetu ambao wataishi na matokeo ya kile ambacho tunafanya au tunajizuwia kukifanya leo. Ndio maana ninatumia nguvu zangu zote kuhakikisha kwamba Ujerumani inachangia kwenye mazingira, uchumi, na jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Sheria iliyopitishwa inajenga mfumo wa utekelezaji wa haya.

Ofisi ya Merkel ambako anatolea salamu zake za Mwaka MpyaPicha: picture-alliance/Global Travel Images/Juergen Held

Tunaweza kujenga juu ya kile kinachotufanya madhubuti: mawazo yetu, akili zetu, kujitolea kwetu, wahandisi wetu, wabunifu wetu, wataalamu wetu, serikali yetu, mifumo ya kujitolea kwetu, utaratibu wetu wa kuishi pamoja mkwenye familia na jumuiya. Kuwashukuru wale wanaofanya kazi ya kuwahudumia wengine.

Na tunaungwa mkono na maadili yanayoelezwa na katiba yetu kuhusu uhuru, mshikamano na heshima kwa utu wa kila mtu na pia misingi ya uchumi wa soko la kijamii. Misingi itabakia kuwa dira yetu kwa muongo ujao. Hii inamaanisha kwamba hata kwenye zama hizi za dijitali, teknolojia inapaswa kuwatumikia watu  na sio kinyume chake. Heshima ya kibinaadamu imeweka mipaka ambayo haiwezi kukiukwa.

Huo ndio msingi wa demokrasia yetu ambao lazima utekelezwe kwenye maisha ya kila siku. Nawashukuru wanawake na wanaume wanaobeba dhima za kisiasa kwenye nchi yetu, hasa wale wanaochanguliwa kwenye serikali za mitaa. Nyinyi kama watu wote nchini mwetu, muko dhidi ya chuki, uhasama na ghasia, ubaguzi na chuki dhidi ya Mayahudi. Kuwalinda watu wote ni jukumu la dola, ni jukumu la serikali kuu ya Ujerumani kujiona kwamba inatimiza wajibu huu.

Nawashukuru wengi wanaofanya kazi kwenye nchi yetu, wale wanaofanya kazi muda wote na wale wanaojitolea: maafisa wa polisi, wazimamoto na wale wanaowasaidia wanaadamu wenzao walio kwenye hali ngumu. Hawa wote ni uti wa mgongo wa demokrasia yetu.
Wapenzi wananchi wenzangu, 

Kwa miaka michache iliyopita mara kadhaa nimesema kwamba Ujerumani itakuwa njema tu endapo Ulaya nzima itakuwa njema pia. Kwa kuwa ni ndani ya Muungano wa Ulaya tu, ndipo tunapoweza kuthibitisha maadili na maslahi yetu na kupata amani, uhuru na maendeleo. Ulaya lazima iwe na sauti zaidi duniani. Tutahakikisha hilo wakati Ujerumani ikichukuwa urais wa Muungano wa Ulaya mwakani, kwa mfano, kupitia mkutano wa kilele kati ya mataifa ya Ulaya na China na mkutano na mataifa ya Afrika.

Kushirikiana na Afrika ni jambo ambalo pia lina maslahi kwetu, kwa sababhu ikiwa watu wana fursa yamaisha ya amani na salama huko waliko, basi idadi ya wakimbizi na wahamiaji itapunguwa. Usalama endelevu utakuja tu ikiwa tutakomesha vita kupitia njia za amani. Usalama na maendeleo yetu unategemeana kwa kiasi kikubwa na ukweli kwamba kwa jirani yetu nako kuko salama na uchumi wake unakuwa. Hii ndio sababu ningelipenda kuwashukuru wanajeshi na maafisa wetu wa polisi wanaofanya kazi hadi nyakati za usiku kwa ajili ya amani yetu.

Wapenzi wananchi wenzangu,

Muongo mpya upo mbele yetu. Miaka ya 20 itakuwa mema. Tujishangaze wenyewe kwa yale tunayoweza kuyafanya. Mabadiliko kwa ajili ya kesho iliyo njema yanawezekana ikiwa tutajihusisha na mambo mapya kwa uwazi na kwa nguvu. Kwa mintarafu hiyo, nawatakieni nyinyi na familia zenu muingie mwaka mpya wa 2020 mukiwa na afya, furaha na baraka tele.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW