Merkel akamilisha ziara yake China
25 Mei 2018Eneo hilo ni makao mkuu ya kampuni za teknolojia ya hali ya juu za China kama Huawei na pia kampuni za kigeni.
Katika ziara hii, Kansela Merkel atashuhudia uvumbuzi wa China katika sekta za magari ya kujiendesha yenyewe na ujasusi unaofanywa na mashine. Kampuni 600 za Ujerumani zinafanya kazi katika mkoa wa Guangdong, ambako ndiko uliko mji wa Shenzhen.
Merkel amekutana na Gavana wa Guangdong Li Xi na akahudhuria kufunguliwa kwa kituo cha uvumbuzi kilichoanzishwa na Chama cha Wafanyabiashara cha Ujerumani walioko nje wa nchi. Kansela huyo amesema Ujerumani itashirikiana na China katika masuala ya teknolojia mpya ila la muhimu kwa jambo hilo kufanyika ni ulinzi mzuri wa data.
Merkel ataitembelea kampuni ya Siemens pia
Merkel amesema alizungumza kwa kina na viongozi wa China jana kuhusu sheria ya mtandao ya nchi hiyo, ambayo wakosoaji wanasema haitoi ulinzi wa kutosha wa data.
Kansela huyo wa Ujerumani pia ataitembelea kampuni ya Siemens ambayo inatengeneza vifaa vya kidijitali vinavyotumika hospitali. Siemens inaajiri jumla ya wafanyakazi 32,000 nchini China.
Hata hivyo, ziara hii ya siku mbili nchini China imefunikwa na mizozo inayoizunguka Iran na Korea Kaskazini. Kufikia sasa, bado Merkel hajatoa auli yoyote kuhusu uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kuyafutilia mbali mazungumzo yaliyokuwa yamepangiwa kufanyika mwezi ujao na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un. Ujerumani na China jana ziliahidi kuunga mkono mpango wa nyuklia wa Iran na kutaka mazungumzo na Korea Kaskazini yaendelee.
Katika mkutano wao na wanahabari, Waziri Mkuu wa China Li Keqiang na Merkel walisema kwamba makubaliano ya Iran hayako makamilifu ila mustakabali wa yale yanayopendekezwa kuwa mbadala si mzuri.
Ziara hii ndiyo ya kwanza ya Merkel China tangu aunde serikali mpya
"Makubaliano yale si makamilifu, ila hakuna makubaliano mengine mazuri. Kwa hiyo, ni lazima tuendelee kuyatekeleza makubaliano hayo. Iwapo Marekani itaweka vikwazo zaidi, baadhi ya makampuni ya Ulaya yatalazimika kujiondoa kutoka Iran," alisema Merkel, "na kutoa nafasi kwa makampuni mengine kutoka maeneo mengine kuingia kwenye soko, ikiwemo China. Haya ni kwa sababu ya maslahi ya China na sitaki kuwazungumzia, lakini sote tunataka kuendelea na makubaliano yaliyoko sasa," aliongeza Kansela huyo wa Ujerumani.
Ziara ya Merkel nchini China ndiyo ya kwanza tangu aunde serikali mpya. Inakuja baada ya kuizuru Marekani kukutana na Trump kisha akaelekea Urusi pia kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin.
Kabla ziara ya China, Merkel alisema, licha ya msimamo mmoja wa Ujerumani na China kuhusu biashara na Iran, ataishinikiza China ili Ujerumani ipate kuingia katika soko lake ambalo linaongozwa pakubwa na serikali na viwanda vingi vimefungia milango washindani kutoka nchi za nje. Hiyo ndiyo sehemu moja ambayo Ujerumani na Marekani zinakubaliana kwamba China inakwenda kinyume ya dhamira yake ya biashara huru.
Mwandishi: Jacob Safari/APE/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef