1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akutana na Hollande mjini Berlin

Admin.WagnerD24 Agosti 2015

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wanakutana Berlin Jumatatu (24,08.2015) kujadili msimamo wa pamoja kwa juhudi za Ulaya kukabiliana na mzozo mkubwa wa wahamiaji kuwahi kushuhudiwa tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Berlin. (24.08.2014)
Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Berlin. (24.08.2014)Picha: T. Schwarz/AFP/Getty Images

Takriban wahamiaji wengine zaidi 2,000 wameingia Serbia usiku wa Jumapili wakitokea Macedonia ambayo imetangaza hali ya hatari kutokana na mmiminiko mkubwa wa wahamiaji wanaoshinikiza kuingia nchini humo kutoka kwenye mpaka wa Ugiriki.

Shirika la Umoja wa Ulaya linaloshughulikia usalama wa mipaka Frontex limesema wiki iliopita limerekodi wahamiaji 107,000 kwenye mipaka yake ambapo 20,000 waliwasili Ugiriki pekee wiki iliopita.

Wakati wahamiaji wengi wakitaka kuvuka na kuingia Macedonia wakitokea Ugiriki serikali ya Macedonia ilifunga mpaka wake kwa siku tatu na polisi walitumia maguruneti ya mshtuko kuwazuwiya mamia ya wakimbizi waliokuwa wakijaribu kuuvunja uzio wa senyen'ge kabla ya kuwaruhusu tena kuingia nchini humo.

Wahamiaji zaidi wawasili

Mjini Rome maafisa wa serikali ya Italia wanasema walinzi wa mwambao wamewaokowa wahamiaji 4,000 kutoka mashua 22 katika bahari ya Mediterenia hapo Jumamosi kwa kile kinachoonekana kuwa idadi kubwa kabisa kwa siku moja kushuhudiwa kwa miaka mingi.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Berlin. (24.08.2014)Picha: T. Schwarz/AFP/Getty Images

Inabidi kuwepo msukumo mpya ili kwamba kile klichoamuliwa kitekelezwe duru kutoka ofisi ya rais nchini Ufaransa imesema hivyo ikikusudia maazmio ya Umoja wa Ulaya yaliofikiwa mwezi wa Juni.

Duru hiyo imesema hali hiyo haijitatuwi yenyewe na kwamba maamuzi yaliofikiwa na Umoja wa Ulaya hayatoshi,yanaburuza miguu na hayana uwezo kukabiliana na hali hiyo.

Orodha maalum

Ufaransa na Ujerumani zinauhimiza Umoja wa Ulaya kuandaa orodha ya nchi ambapo rai wao hawatohesabika kuwa watafuta hifadhi isipokuwa kwa mazingira maalum binafsi.

Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maziere.Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema Umoja wa Ulaya inabidi ukubaliane juu ya orodha ya nchi salama wanakowasili kwanza wahamiaji ili kurahisisha kuwarudisha makwao wakimbizi yakiwemo mataifa yanayojaribu kujiunga na Umoja wa Ulaya na baadhi ya mataifa ya Afrika.

Waziri de Maiziere amekaririwa akisema "Tunahitaji kuwa na ibara ya Ulaya ya kile kinachojulikana kama nchi salama wanakowasili kwanza wahamiaji.Kwa mfano kila nchi inayoomba kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya ihesabiwe kuwa miongoni mwa nchi hizo salama na tunapaswa kuzizingatia baadhi ya nchi za Kiafrika wanko wasili kwanza wahamiaji kuwa ni nchi salama."

Wahamiaji wanatakiwa kupokelewa na kusajiliwa hapo na kurudishwa makwao au iwapo wanahitaji kulindwa kama wahamiaji kutoka Syria wanapelekwa Ulaya."

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa watajaribu kusaidia kuharakisha uanzishaji wa vituo vya kuwapokea wahamiaji katika nchi zilizoelemewa na mzigo huo wa wahamiaji Ugiriki na Italia kusaidia kuwajuwa watafuta hifadhi na wahamiaji haramu.

Nchi hizo zinaona kutokuwepo kwa vituo hivyo na mshikamano Umoja wa Ulaya kurudishwa makwao kwa wahamiaji kutakakopelekea kukatisha tamaa wahamiaji wapya hakutoweza kutekelezwa.

Mbali na mzozo huo wahamiaji Merkel na Hollande pia watajadili kuibuka upya kwa matumizi ya nguvu Ukraine.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW