1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akutana na Rais wa Ghana Akufo-Addo

30 Agosti 2018

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anakutana na Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana mjini Accra, katika siku ya pili ya ziara ya Afrika Magharibi, inayolenga kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kudhibiti uhamiaji haramu.

Ghana - Angela Merkel und Präsident Nana Akufo-Addo
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Uimarishaji wa maendeleo ya kiuchumi barani Afrika ni suala la kipaumbele kwenye ajenda ya sera ya kigeni ya Ujerumani, ambapo Merkel alisema katika ujumbe wa vidio kabla ya kuanza ziara yake hii kwamba ni muhimu kwa mataifa mengi ya Afrika kwa sababu kuna vijana wengi sana barani humo wanaotafuta ajira na mafunzo.

Harakati hizo za kidiplomasia barani Afrika, ambazo zimehusisha ziara nchini Mali, Niger, Ethiopia na Misri kwa kansela huyo wa Ujerumani mwaka 2016, zinaweza kuwa muhimu kwa mustakabali wa kisiasa wa Merkel kwa sababu zinaunda msingi wa mkakati wake wa kukabiliana na visababishi vya uhamiaji na ukimbizi.

Kansela Merkel alipokaribishwa na rais wa Senegal Macky Sall mjini Dakar siku ya Jumatano Agosti 29, 2018.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Merkel amepoteza uugwaji mkono wa kisiasa tangu alipochukuwa uamuzi wa kuwakaribisha mamia kwa maelfu ya wahamiaji nchini Ujerumani, na chama chake cha Christian Democratic Union, CDU, kiko katika nafasi dhaifu sana kuliko ilivyowahi kutokea katika historia yake ya miongo sita.

Akiwa nchini Senegal, alizungumzia haja ya kukabiliana na uhamiaji haramu na wanaofanya biashara ya usafirishaji binadamu.

"Hatuwezi kuwa washiriki wa wasafirishaji haramu wa watu. Hatuweza kukaa na kuangalia watu wakihatarisha maisha yao katika bahari ya Mediterrania. Ndiyo maana ziara hii na ujumbe nilioambatana nao ni muhimu," alisema Merkel katika mkutano wa pamoja na rais wa Senegal, Macky Sall.

Masuluhisho ya Waafrika wenyewe

Rais Sall, ambaye alitangaza mradi wa umeme wa jua katika vijiji 300 utakaofadhiliwa na Ujerumani, alielezea kusikitishwa kwake na hatma ya wahamiaji wanaopoteza maisha wakati wanavuka jangwa la Sahara na bahari ya Mediterrania, na kutoa wito wa kutafuta suluhisho na kubuniwa kwa fursa kwa vijana barani Afrika kwenyewe.

"Siyo kazi ya vijana wa Kiafrika kufia katika bahari ya Mediterrania au mito ya Ulaya au kuishi kwa kujificha," alisema rais Sall wakati akilaani mitandao ya wasafirishaji na wahalifu wanaotengeneza pesa kutoka kwa vijana hao.

"Iwapo tutaweza kuleta maji, umeme, malori na kujenga mazingira ya kuishi, watu hawatahitaji kuondoka nyumbani kwao kwenda kutafuta maisha Ulaya. Hivyo, jawabu la kweli, ni kwa Afrika kutafuta masuluhisho, na Ulaya ina kila sababu ya kutusaidia katika hili. Ni bora kuchukuwa hatua kuliko kumpata daktari baada ya kifo."

Merkel ataizuru pia Nigeria Ijumaa 31.08.2018 na atakutana na Rais Muhammadu Buhari.Picha: imago/R. Zoellner

Uwekezaji barani Afrika

Senegal na Ghana ni miongoni mwa mataifa yenye utulivu na yaliostawi zaidi katika kanda ya Afrika Magharibi, yakiwa na pato jumla la ndani la karibu asilimia 7 na zaidi ya asilimia 8 mtawalia. Merkel anatumaini kuzisaidia nchi hizo kama vituo vya shughuli za kiuchumi.

Licha ya hayo, Berlin pia inataka kukabiliana na China kama mmoja ya mataifa yanayowania kuwekeza katika mataifa yanayoinukia barani Afrika. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan pia aliitembelea Senegal hivi karibuni kujadilia uwekezaji wa moja kwa moja.

Shirikisho la wafanyabiashara wa Ujerumani lenye ushawishi mkubwa BDI, lilisema Merkal anapaswa kuondoa vikwazo vyote vya kibiashara kati ya Ujerumani na Afrika.

Siku ya Ijumaa Merkal ataelekea Nigeria, kukutana na rais wa jumuiya ya kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi - ECOWAS, Jean-Claude Brou. Pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Muhammadu Buhari kuhusu maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini humo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae.

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW