1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel alihutubia bunge baada ya kuondoa vizuizi vya Pasaka

Sylvia Mwehozi
25 Machi 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amelihutubia bunge mchana huu, siku moja baada ya kukataa wito wa kura ya kutokuwa na imani na serikali yake

Deutschland | Bundestag | Angela Merkel gibt Regierungserklärung ab
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Wabunge kutoka chama cha kiliberali cha Free Democratic Party FDP walikuwa wameitisha kura ya kutokuwa na imani baada ya serikali kutangaza mapendekezo ya vizuizi vikali wakati wa sikukuu ya Pasaka. Siku ya Jumatano, Merkel alibatilisha uamuzi huo na kusema kwamba yeye binafsi ndiye anahusika na mpango huo uliokuwa na makosa.

"Nina hakika kabisa kwamba tutavishinda virusi hivi kwa pamoja. Barabara ni ngumu na yenye miamba. Itakuwa na mafanikio lakini pia na makosa. Lakini virusi vitakuwa na kitisho kidogo, na hadi wakati huo lazma tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa mfumo wetu wa afya unaweza kuhimili mzigo mkubwa, wakati huohuo pia tukitathmini athari kubwa ya kiuchumi, elimu, utamaduni na mfumo wetu wa maisha kwa pamoja," alisema Merkel.

Chama cha Social Democrats SPD ambacho ni mshirika mdogo katika muungano wa Merkel wa vyama vya CDU na CSU, nao walimuunga mkono Merke pia wakikataa uwezekano wa kura ya kutokuwa na imani na serikali. Merkel alisema awali kuwa visa vya maambukizi vinaongezeka sio tu Ujerumani bali Ulaya nzima.

Kansela Merkel akihutubia bungeni Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Pia alitetea ugavi wa pamoja ambao Umoja wa Ulaya uliufuata ili kuhakikisha kuna usambazaji sawa wa chanjo kwa nchi wanachama wa Umoja huo. Kansela huyo alionyesha umuhimu wa kikosi kazi cha chanjo cha Umoja wa Ulaya kuongeza ugavi wa dozi katika umoja huo wakati Uingereza ikizalisha chanjo yake binafsi na Marekani haiuzi chanjo nje.

Ujerumani inapambana kukabiliana na wimbi la tatu la maambukizi ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa zaidi na aina mpya ya virusi vya B117 COVID-19. Hii leo taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch imeripoti zaidi ya visa 22,000 vya mamabukizi mapya.

Mpango wa vizuizi vya sikukuu ya pasaka vilitangaza baada ya kumalizika mkutano baina ya kansela Merkel na wakuu wote wa majimbo 16 ya Ujerumani Jumanne wiki hii. Viongozi hao walipanga kuondoa hatua za kulegeza masharti pamoja na kutekeleza hatua kali za siku tano wakati wa sikukuu ya Pasaka ambazo zingeshuhudia maduka yote yakifungwa isipokuwa tu siku moja.

Mpango huo ulikuwa na lengo la kupunguza maambukizi, lakini ulipingwa na wataalamu wa magonjwa waliosema usingeweza kuleta mabadiliko makubwa na hata viongozi wa wafanyabiashara waliodai kuwa ulikuwa wa gharama kubwa na usio na haki.

Muungano wa kihafidhina wa Merkelumekuwa ukiporomoka kwenye kura za maoni za hivi karibuni, kabla ya uchaguzi mkuu wa hapo mwezi septemba. Kutoridhika na kampeni ya utoaji chanjo na kuendelea kwa vizuizi vya COVID-19 pamoja na kashfa kadhaa za ufisadi kumeviathiri vyama vya CDU na CSU huko Bavaria.