1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel alivyoibuka baada ya sakata la wakimbizi

11 Septemba 2017

Miaka miwili baada ya kufungua mipaka na kuwaruhusu maelfu ya wakimbizi kuingia nchini Ujerumani na kupelekea umaarufu wake kushuka, kansela Angela Merkel amepanda tena kutoka shimo refu zaidi la maisha yake ya kisiasa.

Deutschland Flüchtling macht Selfie mit Merkel in Berlin-Spandau
Picha: Reuters/F. Bensch

Karibu mwishoni mwa hotuba yake ya kampeni akiwa kaskazini mwa Ujerumani, Kansela Angela Merkel aliugeukia mgogoro wa wakimbizi wa Ulaya wa mwaka 2015 na kutoa  ujumbe wa aina mbili kwa hadhira.

Wajerumani wanapaswa kujivunia mapokezi waliowapa mamia kwa maefu ya watafuta hifadhi, wengi wao wakikimbia vita na mateso katika kanda ya Mashariki ya Kati, aliuambia mkutano uliohudhuriwa na zaidi ya watu 1,000 katika kijiji cha uvuvi cha Steinhude.

Na kisha akabadili gea: Kilichotokea mwaka 2015 hakiwezi, na hakipaswi kurudiwa tena, alisema. Ni matamshi alioyatumia mara kwa mara katika viwanja vya masoko nchini kote Ujerumani wakati akifanya kampeni za kuchaguliwa kwa muhula wa nne katika uchaguzi mkuu unaofanyika hapo Septemba 24, ambao anatazamiwa kuushinda.

Sababu za Merkel kutoka shimo la kisiasa

Zipo sababu kadhaa zilizopelekea umaarufu wake kupanda tena. Lakini muhimu zaidi ni ujuzi wake wa kucheza na maelezo kuhusu mgogoro wa wakimbizi ambayo Wajerumani wengi wanaweza kuunga mkono, iwe walishangilia au kukosoa matendo yake mwaka 2015.

Watu wakimsikiliza kansela Angela Merkel wakati wa mkutano wake wa kampeni katika mji wa Wolgast, Ujerumani, Septemba 8,2017.Picha: Reuters/F. Bensch

Robin Alexander, mwandishi wa kitabu kilichojipatia umaarufu kuhusu namna serikali ya Ujerumani ilivyoshughulikia mgogoro wa wakimbizi, anasema Merkel hagombei kwa sera ya mipaka wazi na hilo linaendana vizuri na hali iliopo nchini kwa sasa.

Anasema watu wengi wanapenda taswira ya Ujerumani kama ruwaza ya maadili ya kiutu. Na wakati huo huo wanajua nchi yao inaweza kuendelea kuwakaribisha wakimbizi kama ilivyofanya, na ni hisia hizi ambazo Merkel anacheza nazo.

Kufikia mwishoni mwa 2015, waomba hifadhi 890,000 walikuwa wameingia Ujerumani, wengi wao bila kupitia ukaguzi sahihi wa utambulisho, na kuzielemea jamii za wenyeji.

Mwaka mmoja baada ya uamuzi wake, na kufuatiwa na mashambulizi kadhaa madogo madogo ya wafuasi wa itikadi kali, umaarufu wake ulishuka kwa nukta 30 hadi asilimia 45 na alikabiliwa na masuali kuhusu iwapo atawania nafasi ya kansela kwa mara nyingine.

Licha ya hayo, hii leo asilimia 63 ya Wajerumani wanasema anafanya kazi nzuri, kulingana na utafiti wa wakfu wa Bertelsmann wa wiki hii, na asilimia 59 wanaamini nchi iko kwenye mwelekeo sahihi.

Brexit na ushindi wa Donald Trump

Merkel amesaidiwa na matukio ya nje kama vile kura ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya mwaka uliopita na ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani mwaka 2016, matukio ambayo yalishadidia mvuto wake kama mdhamini wa utulivu.

Lakini wepesi wa Merkel kuwaelewa vilivyo wajerumani umemsaidia pia. Katika mikutano yake kadhaa, amekuwa akikabiliwa na waandamanaji wanaopinga uhamiaji wanaojaribu kuvuruga mikutano yake kwa kupiga miluzi na kelele za Merkel laazima aondoke. Lakini waandamanaji hao wamekuwa wakizidiwa nguvu na wafuasi wanaosifu ujumbe wake.

Jambo lingine linalomnufaisha Merkel ni ukweli kwamba vyama vingi vikongwe, kikiwemo chama cha SPD kinachoongozwa na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huu Martin Schulz, viliunga mkono sera yake ya milango wazi.

Chama cha siasa kali za kizalendo cha AfD kinachoendesha kampeni yake kwa misingi ya ubaguzi wa rangi, kimewakasirisha baadhi ya wapigakura na umaarufu wake umeshuka kutoka kiwango kilichofikia mwaka 2016.

Waandamanaji wakiwa na mabango yenye ujumbe usemao: Merkel laazima aondoke, kabla ya mkutano wake wa kampeni mjini Wolgast, Ujerumani, Septemba 8,2017.Picha: Reuters/F. Bensch

Sababu kuu lakini ya kupanda tena kwa umaarufu wa Merkel ni kupungua kwa idadi ya waomba hifadhi wanaoingia nchini Ujerumani. Merkel anasifiwa kwa hili, akiainisha makubaliano alioyaongoza kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, ambayo chini yake idadi ya wahamiaji wanaovuka kuingia Ulaya kupitia ardhi yake imepungua.

Lakini wakosoaji wanasema kufungwa kwa njia ya Balkan, hatua ambayo Merkel alikuwa anaipinga, ndiyo sababu hasa ya kupungua kwa idadi ya wakimbizi.

Wengine wanamfanyia kazi zake chafu

Baadhi wanaona ulinganifu na tabia yake wakati wa mgogoro wa kifedha wa kanda ya euro, wakati rais wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi alipoahidi kufanya kila liwezekanalo kuibakisha kanda hiyo ya sarafu pamoja, na hivyo kumruhusu kuendelea na msimamo wake mkali kuelekea mataifa ya euro kama vile Ugiriki bila kuhofia madhara.

Na katika mgogoro wa wakimbizi, ni mataifa kama Macedonia, Uturuki na Hungary - yaliofunga njia walizokuwa wanatumia wakimbizi - yaliofanya kazi chafu ya Merkel, na kumruhusu kubakisha sura ya kiongozi anaejali, ambaye aliwasaidia watu wanaokimbia vita.

Mkakati huu umemsaidia Merkel kuimarisha udhibiti wake wa siasa za mrengo wa kati. Baadhi ya wapigakura wa mrengo wa kulia wanaweza kuwa walikimbilia chama cha AfD, lakini uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa wapigakura vijana, na wa mijini wanaoegemea upande wa kushoto kiasili wanaweza kujaza pengo hilo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri. Saumu Yusuf