1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel amjibu Trump kuwa Ujerumani si mateka wa Urusi

Sylvia Mwehozi
11 Julai 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekutana na rais Donald Trump pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya kujihami NATO, ambapo Trump amesisitiza kuwa na mahusiano mazuri na Merkel.

Brüssel Nato-Gipfel - Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/F. Mori

Viongozi hao wawili wamekuwa na mazungumzo pembezoni mwa mkutano wa kilele wa NATO unaofanyika mjini Brussels Ubelgiji, saa chache baada ya Trump kuikosoa vikali sera ya Ujerumani juu ya matumizi ya ulinzi na kununua gesi kutoka Urusi.

Mazungumzo yao katika mkutano na waandishi wa habari yalionekana kuwa ya kibiashara zaidi, baada ya Trump kusema Ujerumani inadhibitiwa na Urusi. "Tumekuwa na mkutano mzuri, tumejadili juu ya matumizi ya kijeshi, tukazungumzia biashara", Trump aliwaeleza waandishi wa habari.

Ameongeza kwamba, ana mahusiano mazuri na Merkel pamoja na Ujerumani, na kwamba ameibua wasiwasi wake kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Urusi hadi Ujerumani. Kwa upande wake Merkel amewaeleza waandishi wa habari kuwa wamejadiliana juu ya uhamiaji na biashara na kwamba anatazamia mazungumzo zaidi kama hayo siku za usoni mnamo wakati Marekani inasalia kuwa mshirika wa Ujerumani.  

Rais Donald Trump akiwasili mjini Brussels kwa ajili ya mkutano wa kilelePicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Mkutano wa kilele wa siku mbili ulioanza leo Jumatano, ulitakiwa kuleta mshikamano na ufumbuzi wa kitisho kinacho onekana kuwa cha dunia Urusi. Lakini mazungzmzo yao yanatarajiwa kufunikwa na hoja za Trump kwamba nchi yake inalipa zaidi katika matumizi ya ulinzi wa Ulaya.

Trump awali aliishutumu Ujerumani akisema "inadhibitiwa kikamilifu" na Urusi kutokana na mpango wa ujenzi wa bomba la Nord Stream 2, ambalo litasambaza gesi asilia ya Urusi, alipokutana na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg.

Merkel amemjibu Trump hata hivyo kwamba Ujerumani inafanya maamuzi yake yenyewe, akirejelea nyakati ambazo suala hili halikuwa na uzito.

"Ningependa kuchukua fursa hii kuzingatia matukio ya hivi karibuni, kwamba mimi mwenyewe nilishuhudia baadhi ya  maeneo ya Ujerumani yaliyokuwa chini ya udhibiti wa Urusi na nina furaha sana kuwa leo tuna umoja kwa uhuru kama Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani. Na ndio maana tunaweza kusema kwamba tunafanya siasa zetu wenyewe na kufanya maamuzi yetu wenyewe. Hiyo ni nzuri sana, hasa kwa watu katika nchi mpya ya shirikisho, " alisema Merkel.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg Picha: Reuters/P. Hanna

Washirika wa Jumuiya ya kujihami NATO wameahidi kuongeza bajeti za matumizi ya ulinzi hadi asilimia 2 ya pato la bdihaa za ndani, lengo ambalo litafikiwa na nchi nane pekee ndani ya mwaka huu. Marekani inatarajiwa kuongoza kwa matumizi ya asilimia 3.5 mwaka huu, huku Ujerumani ikitumia asilimia 1.24.

Kauli hizo za bezo zinakuja kuelekea mkutano wa ana kwa ana baina ya Trump na rais wa Urusi Vladimir Putin utakaofanyika siku ya Jumatatu. Merkel pia ametupilia mbali madai ya Trump ya kwamba Ujerumani haitimizi ahadi yake ya matumizi ya ulinzi katika NATO, akibainisha kuwa kufikia mwaka 2024, Ujerumani itakuwa imetumia asilimia 80 zaidi kwenye ulinzi kuliko mwaka 2014.

Naye waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amesema wamezoea ukosoaji unaotolewa na Trump na wanaweza kukabiliana nao.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW