1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aonya kuhusu kusambaratika kwa siasa za dunia

Daniel Gakuba
16 Februari 2019

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amotoa onyo kali dhidi ya kuuachia muundo wa siasa za dunia kusambaratika, na kutoa mwito ya kuinusuru mikataba ya kimataifa ambayo Marekani imeipa kisogo.

MSC München Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Imago/photothek/F. Gärtner

Akihutubia mkutano wa kimataifa kuhusu usalama unaofanyika mjini Munich, Bi Merkel amesema ''hatuwezi kuiacha (mikataba hiyo) ivunjike na kusambaratika'' kwa sababu ipo mizozo mingi inayoikabili dunia.

Kauli ya Kansela Merkel ambaye atastaafu baada ya muhula wake kumalizika mwaka 2021, imechukuliwa kama karipio kwa hatua za Rais wa Marekani Donald Trump. Hotuba yake ndefu imeonekana kama kilele cha mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa nchi na wa serikali wapatao 30, na imeshangiliwa sana na washiriki.

Merkel ameuangazia mkataba kati ya Urusi na Marekani kuhusu makombora ya nyuklia ya masafa ya kati (INF) ambao Marekani imesema itajiondoa rasmi mwezi August, akisema hatua hiyo ya Marekani ilikuwa ''haiepukiki''. Marekani imeishutumu Urusi kukiuka mkataba huo, shutuma ambazo Urusi imekuwa ikizikanusha.

Kushirikishwa kwa China

Makamu Rais wa Marekani Mike Pence ambaye hakukubaliana na Kansela MerkelPicha: Reuters/M. Dalder

Kansela huyo wa Ujerumani ametaka China ijiunge katika mazungumzo yatakayoweka mkataba mpana zaidi katika misingi ya INF, akisema kudhibiti mashindano ya kutengeneza silaha za maangamizi ni suala lililoihusu kila nchi.

Wakati umoja wa kujihami wa NATO ukikosolewa vikali na Rais Donald Trump, Angela Merkel amesisitiza umuhimu wa washirika ''kuimarisha kufanya kazi pamoja katika sekta mbali mbali, ya ulinzi ikiwemo.''

Amezungumzia vile vile makubaliano ya mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ambayo Marekani imeyatupilia mbali, akisema ingawa upo muafaka kwamba Iran inapaswa kudhibitiwa, kuna tofauti kuhusu namna ya kutekeleza lengo hilo.

Bomba la mafuta kati ya Urusi na Ujerumani

Maafisa wa Ujerumani na Urusi wakikutana pembezoni mwa mkutano wa usalama wa MunichPicha: picture alliance/dpa

Suala jingine aliloligusia Kansela Merkel katika hotuba yake ni mzozo kuhusu ujenzi wa bomba la gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani, maarufu kama Nord Stream 2, ambao unapingwa vikali na Marekani pamoja na baadhi ya nchi za Ulaya, hususan za Ulaya ya Kati, Amesema haoni tofauti ya gesi itokayo Urusi kupitia bomba hilo, na inayokuja kwa bomba linalopita nchini Ukraine, ambalo halipigiwi kelele.

''Ikiwa tulikuwa tukiagiza kiasi kikubwa cha gesi ya Urusi wakati wa vita baridi, kitu gani kimekwenda kombo kwa kiwango cha kusema sasa hatuwezi kuichukulia nchi hiyo kama mshirika?'' Ameuliza Merkel.

Wito wa Kansela Merkel wa ushirikiano wa kimataifa umepingwa na Makamu Rais wa Marekani Mike Pence ambaye vile vile anahudhuria mkutano wa usalama wa Munich. Katika kuendeleza mashambulizi ya utawala wa Rais Donald dhidi ya washirika wa jadi wa Marekani, Pence ameziponda sera za nchi za Ulaya kuhusu Iran na Venezuela.

Amezitaka nchi za Ulaya na za Asia kufuata mfano wa Marekani na kujiondoa katika mpango wa nyuklia wa Iran, na kumtambua Juan Guaido aliyejitangaza rais wa mpito wa Venezuela.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, rtre

Mhariri:Sylvia Mwehozi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW