Merkel aonya Uingereza haitapata upendeleo maalum Brexit
27 Aprili 2017Bi Merkel ameyasema hayo katika bunge la Ujerumani , na kuongeza kwamba taifa ambalo ni mshirika tu halitakuwa na haki kama taifa mwanachama, amesema Merkel kabla ya mkutano mjini Brussels kuhusiana na Brexit siku ya Jumamosi.
"Hii inawezekana kuonekana kama kujipendelea, lakini ni lazima niseme wazi kwasababu baadhi ya watu nchini Uingereza wanaonekana kuwa na ndoto za mchana kuhusiana na suala hili," Merkel amesema bungeni leo...
"Wapenzi ndugu zangu, huenda mnaweza kufikiria kwamba hili ni jambo la kawaida tu. Lakini kwa bahati mbaya naweza kusema wazi kwamba napata hisia baadhi ya watu nchini Uingereza wana mawazo ya kufikirika. Hii ni kupoteza wakati."
Merkel amesema mazungumzo kuanzia mwanzo kabisa ni lazima yajumuishe majukumu ya kifedha ya Uingereza, ikiwa ni pamoja na baada ya kujitoa kutoka Umoja huo. Pia amesema masharti ya kujitoa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya ni lazima yafikiwe katika njia inayoridhisha kabla ya majadiliano kuingia katika uhusiano wa hapo baadaye na Umoja huo, mtiririko ambao Merkel ameuita , usioweza kubadilishwa tena.
Mpango wa majadiliano
"Mpango wa mtiririko wa jinsi tutakavyolishughulikia suala hili uko wazi na hautakuwa hata hivyo kila mara rahisi kuufuata, tunaweza tu kufikia makubaliano juu ya uhusiano wa hapo baadaye na Uingereza mara masuala yote ya kujitoa yatakapotatuliwa kwa njia inayoridhisha. Hii ina maana kwamba ni haraka kiasi gani Uingereza inaweza kufikia suluhisho sahihi, ndipo tutakapoyaangalia matakwa yao ya kuzungumzia suala la uhisiano wa hapo baadaye katika yao na Umoja wa Ulaya katika majadiliano ya kujitoa. Lakini kwanza tunalazimika kufamu ni vipi Uingereza inauona uhusiano wake nasi."
Viongozi wa mataifa mengine 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya watakutana Aprili 29 kuweka misingi ya Umoja huo , licha ya kwamba mazungumzo hayo yataanza rasmi mwezi wa Juni mwaka huu. Umoja wa ulaya umeimarisha mkakati wake , ukitoa madai mapya kuhusiana na huduma za kifedha, uhamiaji na fedha ambazo Uingereza inapaswa kulipa kabla ya kufikisha mwisho uanachama wake katika Umoja huo uliodumu kwa miaka 44.
"Majadiliano ya kujitoa bila shaka yatahitajika kufikiwa kwa makubaliano makubwa baina ya Umoja wa Ulaya pamoja na Uingereza binafsi katika miaka miwili ijayo. Nafikiri hilo halina shaka kabisa."
Uturuki pia yaonywa
Kuhusiana na suala la uhisiano kati ya Umoja wa ulaya na Uturuki , Merkel amesema , uhusiano huo umedhoofika pakubwa kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali ya rais Recep Tayyip Erdogan. Merkel ameeleza wasi wasi wake kwamba kura ya maoni iliyofanyika nchini Uturuki Aprili 16 haikufanywa katika mazingira ya usawa. Ameionya Uturuki kuheshimu haki za raia kwa misingi ya taifa linaloheshimu katiba. Pia amesema atatumia mkutano pamoja na viongozi wenzake wa Umoja wa ulaya mjini Brussels siku ya Jumamosi kujadili hatua za kuchukua kuelekea Uturuki.
Mwandishi: Sekione Kitojo /afpe /dpae
Mhariri: Yusuf , Saumu