Merkel aonyesha matumaini kuhusu Ugiriki
19 Juni 2011Pia amepongeza maendeleo ambayo Ugiriki imeyafikia mwaka mmoja uliopita kuelekea kukabiliana na mzozo wake wa madeni, lakini amesema bado haijatosha.
Ujerumani na Ufaransa zimeahidi kuendeleza msaada wao wa kifedha kwa Ugiriki, lakini Ujerumani inataka wawekezaji binafsi wachangie katika mpango wa pili wa kuiokoa Ugiriki na madeni, ambao utajadiliwa baadae mwezi huu.
Mwenyekiti wa kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro, Jean-Claude Juncker ameionya Ujerumani kutoyashinikiza mabenki binafsi yanayoshikilia hisa katika benki za Ugiriki kuchangia zaidi katika msaada huo.
Amesema hatua hiyo itasababisha mashirika ya uorodheshaji kuitangaza Ugiriki kuwa katika hali ya kutoweza kulipa madeni yake na athari zikiwepo kwa Ubelgiji na Italia.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,DPAE,AFPE)
Mhariri: Maryam Abdalla