Merkel arejea tena katika uchaguzi jimboni Lower Saxony
15 Oktoba 2017Wiki tatu baada ya wapiga kura nchini Ujerumani kukika chama cha kansela Merkel cha Christian Democratic Union matokeo yake mabaya kabisa katika muda wa miongo kadhaa, kiongozi huyo wa nchi yenye uchumi mkubwa kabisa katika Umoja wa Ulaya anakabiliwa na uchaguzi mwingine , mara hii katika jimbo la Lower Saxony.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa majira ya saa mbili asubuhi saa za Ulaya ya kati kwa ajili ya wapiga kura milioni 6.1 walioandikishwa kupiga kura na vinatarajiwa kufungwa saa 12 jioni wakati makadirio ya kwanza yatakapotolewa katika televisheni ya umma.
Uchunguzi wa hivi karibuni wa maoni ya wapiga kura yanaonesha kwamba chama cha CDU kiko nyuma ya chama cha Social Democratic SPD katika jimbo hilo, jimbo la nne kwa idadi ya watu nchini Ujerumani na mahali kilipo kiwanda cha kutengenezea magari ya Wolkswagen kilichokumbwa na kashfa.
"Ushindi katika jimbo la Lower Saxony ni muhimu kwa Merkel kwasababu utamuimarisha na kuonesha kwamba chama chake kinaweza bado kushinda chaguzi za majimbo," amesema Oskar Niedermayer wa chuo huria cha mjini Berlin.
Lakini kushindwa "kutakuwa ishara mbaya kwa ajili ya majadiliano ambayo yanaanza katikati ya wiki ijayo" ya kuunda serikali mpya ya mseto mjini Berlin, gazeti maarufu nchini Ujerumani la Bild limesema leo Jumapili(15.10.2017).
SPD yawania ushindi
Mpizani wa Merkel , kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz , pia anawania kupata ushindi katika uchaguzi huo , baada ya kipingo cha kudhalilisha katika uchaguzi wa taifa.
Jimbo la Lower Saxony limelazimika kufanya uchaguzi wa mapema baada ya muungano uliokuwa ukitawala katika jimbo hilo wa chama cha SPD na chama cha kijani kuvunjika kilipopoteza wingi wake mdogo kutokana na kujitoa kwa mbunge mmoja chamani.
Muungano dhaifu kama huo utakuwa haswa kile Merkel anachotaka kukiepuka wakati akifungua mazungumzo na washirika watarajiwa siku ya Jumatano.
Lakini baada ya miaka 12 madarakani katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa katika Umoja wa Ulaya , sasa anakabiliwa na moja kati ya changamoto kubwa kabisa: kuwabadilisha washirika wa kisiasa ambao ni wapinzani kuwa washirika wenza.
Iwapo atafanikiwa , Ujerumani inaweza kupata serikali yake ya kwanza ya mseto ya kundi la kambi yake ya kihafidhina, waliberali na wanaopendelea biashara chama cha Free Democrats , FDP na chama cha walinzi wa mazingira , cha kijani iwapo watashindwa kufikia makubaliano , Merkel atawajibika kuitisha upya uchaguzi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri Lilian Mtono