1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa lazima ikubali kuzungumza na Taliban

25 Agosti 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel asema ukweli kwamba Taliban wamechukua madaraka Afghanistan ni mchungu, lakini jumuiya ya kimataifa yapaswa kuzungumza nao ili kuyalinda mafanikio yaliyopatikana miaka 20 iliyopita.

Angela Merkel
Picha: Markus Schreiber/picture alliance/AP

Akizungumzia suala la kwanini matukio hayo yamekuwa ya kushangaza kwa jamii ya kimataifa, Merkel amesema kuwa mataifa ya Magharibi yalio na nguvu yalidharau jinsi vikosi vya Afghanistan vingeachilia kwa haraka upinzani wao dhidi ya kundi la Taliban baada ya kuondoka kwa vikosi vya kigeni.

Kwa mtazamo wa nyuma, ilikuwa rahisi kusema nini kinapaswa kufanyika, lakini maamuzi yalipaswa kufanywa wakati matukio yalikuwa yakitokea. Merkel amesema kuwa lengo lao linapaswa kuwa kudumisha kwa kiwango kikubwa mabadiliko waliofanya nchini Afghanistan katika muda wa miaka 20 iliyopita na kwamba anaridhia mashauriano na kundi la Taliban kwa kuwa sasa ndio ukweli wa Afghanistan.

Merkel amesema kuwa kwasasa, serikali inazingatia kikamilifu kuhusu shughuli ya uhamishaji kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kabul ambayo inapaswa kukamilika kufikia Agosti 31 wakati vikosi vya Marekani vinapanga kuondoka nchini humo. Merkel ameongeza kusema. Katika taarifa, Merkel alitoa risala zake kwa wale waliokufa ama kujeruhiwa walipokuwa wakihudumu nchini Afghanistan katika muda wa miongo hiyo miwili na kufichua kuwa mmoja wa walinzi wake wa zamani alikuwa miongoni mwa wanajeshi 59 wa Ujerumani waliouawa katika mapigano hayo.

Wakazi wa Afghanistan katika mchakato wa kuhamishwa kutoka KabulPicha: Staff Sgt. Victor Mancilla/U.S. Marine Corps/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa China Xi Jinping wamekubaliana kwamba mataifa yao yataimarisha juhudi za kukabiliana na vitisho kutoka Afghanistan kufuatia kuchukuliwa kwa uongozi na kundi la Taliban . Haya yamesemwa leo na ikulu ya Kremlin. Katika taarifa, ikulu hiyo imesema kuwa katika mazungumzo kwa njia ya simu, viongozi hao wawili walielezea kujitolea kwao kukabiliana na vitisho vya ugaidi na ulanguzi wa dawa za kulevya kutoka Afghanistan. Pia walizungumzia kuhusu umuhimu wa kutafuta amani nchini Afghanistan na kuzuia kuenea kwa ukosefu wa usalama katika maeneo ya karibu.

Huku hayo yakijiri, uongozi wa Taliban, umewateuwa wanasiasa wakongwe wawili katika nafasi za waziri wa fedha na ulinzi. Kulingana na shirika la utangazaji la al-Jazeera, mmoja wao ni Mullah Abdul Qayyum Zakir, mfungwa wa zamani katika gereza la Guantanamo ambaye ametajwa kuwa kaimu waziri wa ulinzi. Hata hivyo, bado hakuna tangazo rasmi kutoka Taliban kuhusiana na uteuzi huo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW