1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ashinikiza mabadiliko ya sera ya wakimbizi Ulaya

5 Septemba 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametishia kuchukuwa hatua ya kisheria dhidi ya nchi za Umoja wa Ulaya zenye kukiuka makubaliano kuhusu wakimbizi na kusisitiza Ujerumani haitofilisika kutokana na mzozo wa wahamiaji.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Kansela Merkel ametangaza kwamba ataendelea kuwa na mzungumzo mazito na washirika wenzake wa Ulaya kuhusu mzozo wa wakimbizi unaoendela kuisibu Ulaya. Merkel amesisitiza kwamba majukumu yote na mzigo unaohusiana na wimbi hilo la wakimbizi inabidi yagawiwe kwa haki miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ili kuhakikisha nchi hizo zinashirikiana kuubeba mzigo huo.

Akizungumza katika shirika la vyombo vya habari la Funke Mediengruppe katika mji wa Essen amesema sera ya sasa ya Ulaya kwa watafuta hifadhi haifanyi kazi na kusisitiza "mfumo huo mzima inabidi ubadilishwe kabisa."

Hakuna kikomo cha sheria

Kansela huyo wa Ujerumani amesema hakuna kikomo cha sheria kwa idadi ya watafuta hifadhi ambao nchi yake inaweza kuwapokea. Katika mahojiano na magazeti ya ushirika wa vyombo vya habari vya Funcke yaliochapishwa Jumamosi Merkel amesema "haki kwa hifadhi ya kisiasa haina kikomo kwa idadi ya watafuta hifadhi." Amesema ikiwa ni nchi madhubuti yenye nguvu za kiuchumi wana nguvu za kufanya kile kinachohitajika kuhakikisha kila mtafuta hifadhi kesi yake inasikilizwa kwa haki. Lakini Merkel amesisitiza juu ya msimamo wa serikali yake wa kuwarudisha makwao wahamiaji ambao hawana nafasi ya kupata kibali cha kuendelea kubakia.

Wahamiaji wakiwasili Munich Ujerumani kutokea AustriaPicha: Getty Images/A. Beier

Wajibu wa pamoja

Merkel pia amesisitiza kwamba mataifa yote ya Umoja wa Ulaya yanatakiwa kuheshimu makubaliano ya Geneva kuhusu wakimbizi na kurudia tena tishio lake la kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya mataifa yenye kukiuka sera ya uhamiaji ya Ulaya.

Masahibu yaliyowakuta wahamiaji HungaryPicha: Reuters/L. Balogh

Merkel amesema itabidi Ulaya nzima iingie katika majaribu kwa mujibu wa ukubwa na nguvu za kiuchumi za kila nchi. Ametaka wahamiaji wenye uwezekano wa kuendelea kubakia Ulaya washughulikiwe kwa haraka na kugawanywa miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Wasyria wafarajika

Wasyria kadhaa walijitokeza Essen kumshukuru Merkel kwa kukubali kuwapokea wahamiaji kutoka Syria ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe viliodumu kwa miaka mingi vimewalazimisha mamilioni kuikimbia nchi hiyo.

Wahamiaji wakiwa na picha za Kansela Angela Merkel Budapest, Hungary.Picha: Reuters/B. Szabo

Osama Khal ambaye alikuwepo wakati wa ziara hiyo ya Merkel huko Esen amesema wote walikuwa wakitaka kumshukuru Merkel kwa kutangaza kwamba Ujerumani itawapokea wakimbizi wa Syria.

Waandamanaji wa sera kali za mrengo wa kulia pia walihuduria matukio ya hadhara ya ziara hiyo ya Merkel huko Essen na kuingilia kati hotuba yake mara kadhaa kwa kumzomeya. Wanazi mambo leo pia walipeperusha bendera ya tawi la vijana la chama cha sera kali za mrengo wa kulia cha NPD.

Merkel pia alitumia hotuba yake kwa kuzungumzia tatizo la kuibuka kwa wafuasi wa sera kali za mrengo wa kulia kwa kusema Ujerumani iko kwenye tishio jipya la ugaidi kutoka kwa watu waliobadilishwa mawazo na kupachikwa nadharia za ufashisti.

Katika hotuba hiyo Merkel amesema inabidi wawe macho na kuangalia matukio ya hivi karibuni kwa kusimama kidete dhidi yao.

Ameongeza kusema kwamba aibu kama ile ya mfululizo wa mauji yaliofanywa na vuguvugu la kundi la chini kwa chini la NSU haipaswi kurudiwa.Merkel amesisitiza sera yake ya msimamo wa kutovumuliwa kabisa kwa wapandikiza chuki na wenye kuchukia wageni akisisitiza mashambulizi dhidi ya nyumba za wahamiaji na watafuta hifadhi wahusika watashtakiwa kwa nguvu kubwa za kisheria.

Ujerumani kutofiliska kwa wakimbizi

Katika hotuba yake ya kila wiki kwa njia ya mtandao Merkel amesema hapo Jumamosi Ujerumani haitofilisika kama matokeo ya mzozo wa wahamiaji unaoendelea barani Ulaya.

Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: Reuters/D. Balibouse

"Hatuwezi kusema kwa sababu tuna kazi ngumu bajeti yenye urari au suala la nakisi litakuwa tena halina maana." amesema Merkel na kusisitiza uchumi wenye nguvu unamaanisha uwezo mkubwa kwa jamii kuhudumia na kuwapatia makaazi wahamiaji.

Merkel amekuelezea kukubali na kuwajumuisha wakimbizi katika jamii ya Ujerumani kuwa ni kazi ya taifa.Amesema kila ngazi ya jimbo,mitaa na serikali ya shirikisho inabidi itimize wajibu wake na kuongeza kwamba mapato ya kodi katika ngazi zote za serikali yamekuwa mazuri kuliko ilivyotegemewa.

Matamshi yake hayo yanakuja kabla ya mkutano wa kilele wa serikali ya mseto kati ya chama cha sera za wastani kulia cha Merkel CDU na washirika wake wa sera za mrengo wa kushoto SPD.

Wanasiasa wataamuwa katika mkutano wa Jumapili kiasi gani cha fedha kinapaswa kutolewa kwa serikali za mikoa na mitaa kusaidia kukabiliana na idadi kubwa ya watu wanaokuja Ujerumani kutafuta hifadhi.

Bajeti ya vyama hivyo inaruhusu hadi euro bilioni 5 kutolewa kama msaada wa ziada kwa ajili ya mzozo huo wa wahamiaji wakati fedha zitakazotolewa zitaidhinishwa katika mkutano wa kilele na serikali za majimbo hapo Septemba 24.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ Reuters/dpa

Mhariri: Elizabeth Shoo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW