Merkel ashinikiza utawala wa sheria China
12 Juni 2016Merkel amewasili China Jumapili (12.06.2016) huku kukiwa na ongezeko la shinikizo kutoka kwa makampuni na mashirika ya haki za binaadamu kukabiliana na nchi hiyo ipasavyo.
Serikali ya China imekuwa ikikandamiza mashirika na wanaharakati wa haki za binaadamu na inakabiliwa na lawama kutoka kampuni za kigeni kuhusu vikwazo vya masoko.
Akizungumza na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Beijing, Merkel ameelezea umuhimu wa utawala wa kweli wa sheria.
Utawala wa sheria
Amesema hiyo inamaanisha mahakama zitowe hukumu kwa mujibu wa sheria za nchi na bila ya upendeleo wa kisiasa na kwamba kila mtu yuko sawa mbele ya sheria "inamaanisha michakato na hukumu za mahakama inabidi ifanyike kwa uwazi."
Amesema "iwapo zitatekelezwa kwa njia hiyo utawala wa sheria utaimarisha imani ya wananchi kwa asasi za taifa na maamuzi yake na kwa hiyo pia kuimarisha utulivu wa jamii katika nchi."
Mahakama za China zinadhibitiwa na chama tawala cha Kikomunisti juu ya kwamba Rais Xi Jinping anajaribu kuboresha utawala wa sheria na kutaka wananchi wa kawaida watatuwe manu'nguniko yao kwa kupitia mahakamani badala ya kuandamana mitaani.
Haki kwa kampuni za kigeni
Merkel ameongeza kusema kwamba kampuni za kigeni pia zinahitaji kuwa na msingi mzuri wa kisheria kuendesha shughuli zake.
Amesema msingi wa kisheria kwa kampuni inabidi pia usarifiwe kwa njia ya kuziwezesha kampuni za kigeni kufaidika na haki na upendeleo sawa na kampuni za ndani ya nchi kwa mfano kuhusiana na zabuni za serikali,kulinda ipasavyo alama za chapa za makampuni, haki miliki na data.
China mara kwa mara imekuwa ikiahidi kufunguwa nafasi zaidi za masoko kwa ajili ya kampuni za kigeni na kufanya mageuzi ya masoko katika juhudi za kuuchapuwa uchumi wake unaolega lega.
Wakosoaji wa kigeni wanaishutumu nchi hiyo kwa kutotekeleza agenda yake ya mageuzi na badala yake kuanzisha taratibu mpya ambazo zinazidi kuzuwiya nafasi za masoko.
Mzozo wa chuma cha pua
Ziara ya Merekel pia inakuja wakati kukiwa na ghadhabu barani Ulaya kuhusu usafrishaji nje wa chuma cha pua wa China ambao ongezeko lake kubwa limekuja kushutumiwa na washindani wake duniani ambapo wanaituhumu nchi hiyo kwa kuuza kwa bei rahisi za kutupwa baada ya kupunguwa kwa mahitaji nyumbani.
Akigusia suala hilo la chuma cha pua Merkel amesema "inabidi tuhakikishe uwanja wa biashara unakuwa wa haki"Ameongeza kusema "hakuna mtu anayetaka kuona vita hivyo vya biashara kati ya China na Umoja wa Ulaya vinatanuka lakini inamaanisha inabidi tuzungumze juu ya masuala yaliokosa ufumbuzi."
Kansela Merkel yuko China kuhudhuria mkutano wa nne wa Baraza la pamoja la mawaziri kati ya China na Ujerumani na ameongozana na mawaziri sita na makatibu wakuu watano, ambao watakutana na wenzao wa China.
Ujerumani inataka kuimarishwa hatua za kuhami masoko kukabiliana na bei rahisi za kutupwa za bidhaa za China, pamoja na kuitaka China kupunguza uzalishaji wa kupindukia wa chuma cha pua ambao unaongeza shinikizo kwa masoko ya Umoja wa Ulaya na kupelekea wasiwasi kutoka kwa umoja huo.
Mwandishi . Mohamed Dahman/Reuters/dpa
Mhariri : Sylvia Mwehozi