Merkel asisitiza umuhimu wa Umoja wa Ulaya kwa Ujerumani
22 Februari 2018Ulaya imo katika mbinyo kisiasa na kiuchumi duniani kote, Merkel aliwaambia wabunge mjini Berlin hii leo. Ujerumani inaweza kufanya vizuri iwapo Ulaya inafanya vizuri, alisema Merkel na kuainisha umuhimu wa Umoja wa Ulaya kwa Ujerumani. Amesema hayo leo katika bunge la Ujerumani Bundestag kabla ya kufanyika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya ambao utashughulikia bajeti ya hapo baadaye ya mataifa hayo.
Merkel aligusia pia mizozo ya kikanda ambapo alisema Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua jukumu la juu kutatua mizozo na kudokeza haja ya kutatua mzozo nchini Syria.
Kwa jumla kuna mengi ya kufanya katika sera zetu za mambo ya kigeni. mambo hayo ni kuhusu uhusiano wetu na Urusi, China na pia katika jukumu letu la kutafuta suluhisho la mizozo ya kikanda. Katika hali ya kutisha tunayoiona nchini Syria , ambapo utawala wa nchi hiyo haupambani na magaidi, bali na wananchi wake , unaharibu mahospitali na ni mauaji ambayo tunapaswa kuchukua jukumu la kuyazuwia.
Kansela wa Ujerumani amesema kwamba kujitoa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya kunatoa fursa kwa Umoja huo kufikiria kwa upana mfumo wake wa kifedha. Akihutubia bunge la Ujerumani Bundestga, Merkel aliweka wazi kwamba hatma ya Umoja wa Ulaya litakuwa suala la umbele katika muhula wake wa nne madarakani, iwapo makubaliano ya kuunda serikali ya mseto baina kati ya wahafidhina anaowangoza na Wademocrats ambao wanaunga mkono Umoja wa Ulaya utaidhinishwa na wanachama wa chama hicho cha SPD.
Mkutano wa viongozi wa Ulaya
"Tunahitaji mwanzo mpya kwa Ulaya," Merkel alisema , na kuongeza kwamba mjadala unaokaribia juu ya bajeti mpya kwa kundi hilo la mataifa 27 baada ya Uingereza kujitoa mwaka 2019 unaweza kusababisha baadhi ya mabadiliko makubwa.
"Mjadala juu ya hali ya baadaye ya mfumo wa kifedha pia ni fursa ya kuangalia utaratibu wa kifedha wa Umoja wa Ulaya kwa jumla" amesema.
Viongozi katika mkutano wa Ijumaa watajadili iwapo kuimarisha bajeti ya miaka saba ijayo kulipia sera za pamoja katika usalama, ulinzi na uhamiaji kati ya mwaka 2021 hadi 2027.
Ujerumani , ambayo ina uchumi mkubwa barani Ulaya, ni mchangia mkubwa na imesema iko tayari kulipa zaidi licha ya baadhi ya nchi , kama Uholanzi , kudai kuwa kundi dogo la nchi bila ya Uingereza , ina maana ya bajeti ndogo.
Merkel ametaka kuwahakikishia wale miongoni mwa kundi la wahfidhina ambao wana shaka bado juu ya ujumuisho wa ndani zaidi katika Umoja wa Ulaya na kulipia masikini, nchi wanachama ambazo zimezongwa na madeni.
"Mshikamano hauwezi kufuata njia ya upande mmoja," amesema Merkel.
"Mkataba wa uthabiti na na ukuaji utabakia kuwa dira kwa ajili ya Ulaya," amesema , na kuongeza , akisisitiza kwamba mzigo huo na ukaguzi unapaswa kwenda mkono kwa mkono kama sehemu ya mageuzi ya kanda ya sarafu ya euro.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Josephat Charo