1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ataka kudhibiti mmiminiko wa wakimbizi

Iddi7 Januari 2016

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema angependa kuona mmiminiko wa wakimbizi barani Ulaya ukidhibtiwa, na wakati huo mipaka baina ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya ikiendelea kuwa wazi.

Wildbad Kreuth CSU Klausur Hasselfeldt Seehofer Merkel Scheuer
Picha: Getty Images/AFP/J. Simon

Merkel, ambaye Novemba mwaka jana alitimiza muongo mmoja madarakani, anauanza mwaka huu wa 2016 akikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa chama chake mwenyewe, kumtaka apunguze idadi ya watafuta hifadhi wanaowasili Ujerumani, baada ya wakimbizi zaidi ya milioni moja kusajiliwa mwaka jana, hali iliyopelekea kupungua kwa uungaji mkono wa umma kwa kiongozi huyo kuhusu suala la wakimbizi.

Akizungumza kabla ya mkutano mkuu wa chama cha Christian Social Union CSU, chama ndugu na kile cha kwake cha Christian Democratic Union CDU, Merkel alisema wanahitaji kukabiliana na sababu zinazopelekea ukimbizi.

"Kwangu ni muhimu kuwa tunapunguza pakubwa idadi ya wakimbizi kwa kupambana na vyanzo vya uhamiaji lakini pia hatua za kitaifa, kwa mfano njia bora za kuwarudisha waomba hifadhi wanaokataliwa, lakini wakati huo tunalinda uhuru wa watu kutembea ndani ya Umoja wa Ulaya, aliwambia waandishi wa habari mjini Wildbad Kreuth.

Jarida la Time lilimtaja Merkel kuwa 'Mtu wa Mwaka' 2015 kutokana na uongozi wake katika suala zima la wakimbizi.Picha: picture-alliance/AP Photo/Time Magazine

Uhuru huo wa kutembea, ambao umeyapelekea mataifa 26 ya bara la Ulaya kuondoa ukaguzi wa mipakani ndani ya kanda yao ya Schengeni, ulikuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi na mafanikio, alisema Merkel.

Ukaguzi wa mpakani Sweden na Denmark

Jirani wa Ujerumani katika upande wa kaskazini - Denmark, ilirudisha ukaguzi wa muda katika mpaka wake siku ya Jumatatu, ikihofia kwamba inaweza kugeuka kituo cha mwisho kwa wakimbizi wengi baada ya Sweden kuweka vidhibiti kuwazuwia kuendelea zaidi kuelekea kaskazini.

Merkel alitajwa kuwa mtu wa mwaka na jarida la Marekani la Time na pia gazeti la Financial Times la Uingereza, baada ya kuwafungulia milango wakimbizi mwezi Agosti, lakini matokeo ya wimbi kubwa la wahamiaji yamekuwa kuminwya zaidi kwa rasilimali za umma na kuwakasirisha baadhi ya raia.

Wizara ya mambo ya ndani ilisema Jumatano kwamba rekodi ya wahamiaji 476,000 waliomba hifadhi mwaka jana, na maombi ya wengine 600,000 bado kukusanywa. Licha ya kuapa kupunguza idadi yao mwezi uliyopita, Merkel anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa chama cha CSU kuchukuwa hatua zaidi.

Mwenyekiti wa CSU Horst Seehorfer, amependekeza ukomo wa wahamiaji 200,000 kwa mwaka ili kuipunguzia mzigo hazina ya umma na kurahisisha mchakato wa kuwajumuisha wakimbizi hao katika jamii. Seehorfer alisema kabla ya mkutano huo kuwa wastani wa wakimbizi 3000 huingia nchini Ujerumani kila siku.

Akataa kufunga mipaka

Jimbo la Bavaria ndiyo limeathirika zaidi na uhamiaji huu mkubwa, ambapo sehemu kubwa ya wakimbizi milioni 1.1 waliorekodiwa Ujerumani waliingia kupitia mpaka wa kusini wa jimbo hilo. Merkel amekataa miito ya kuwafungia mipaka wakimbizi, ambao wengi wanakimbia vita Mashariki ya Kati au nchini Afghanistan.

Merkel akiwa na viongozi wakuu wa chama cha CSU mjini Wildbad Kreuth, Bavaria.Picha: picture-alliance/dpa/M. Balk

Anahoji kuwa mmiminiko huo unapaswa kushughulikiwa nje ya Ujerumani, kupitia majadiliano ya kumaliza vita nchini Syria, kuihamasisha Uturuki kuboresha mazingira ya wakimbizi walioko huko, na kuwashawishi washirika wa Ulaya kukubali mgawanyo wa watafuta hifadhi.

David Cameron aomba msaada

Mkutano huo wa CSU unahudhuriwa pia na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, ambaye ameiomba Ujerumani imsaidie kufanikisha mageuzi ndani ya Umoja wa Ulaya, ili aweze kuwashawishi wapigakura nchini mwake kuunga mkono kubakia kwa Uingereza katika umoja huo, itakapofanyika kura ya maoni kuamua juu ya suala hilo mwaka ujao.

Merkel amesema anataka mazungumzo ya kujadili upya uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kutoa makubaliano yatakayofanikisha kuibakiza nchi hiyo ambayo ni mwanzilishi wa Umoja wa Ulaya, lakini aliongeza kuwa uamuzi wa mwisho ni Waingereza wenyewe.

Mwandishi. Iddi Ssessanga/dpa,rtre

Mhariri: Bruce Amani

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW