Merkel atembelea jimbo lingine lililokumbwa na mafuriko
20 Julai 2021Akiwa ameambatana na Armin Laschet, waziri mkuu wa jimbo North Rhine Westphalia na mwanasiasa ambaye yumkini atarithi wadhifa wa Ukansela baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba, bibi Merkel ameyazuru maeneo yaliyoshuhudia uharibifu usio na mfano wakati wa mafuriko ya wiki iliyopita.
Kwanza alikitembelea kitongoji cha Bad Muenstereifel katika wilaya ya Euskirchen ambako ameahidi msaada wa dharura kwa watu wote walioathirika na mafuriko na kusisitiza kwamba msaada huo utatolewa katika msingi wa kuepuka urasimu.
Kansela Merkel amewaarifu wahanga wa kadhia ya mafuriko kuwa juhudi zinafanywa kuhakikisha fedha zitawafikia haraka na ikiwezekana ndani ya siku chache zinazokuja. Kiasi Euro milioni 300 kimetengwa kwa ajili ya msaada.
Merkel atoa wito wa mshikamano wa taifa
Akiwa kwenye ziara hiyo ambayo imemwezesha kwa mara nyingine kuona kiwango cha uharibifu wa mali na miundombinu, Kansela Merkel amerejea wito wa mshikamano na kutoa salamu za pole na rambi rambi kwa familia za wahanga wa maafa hayo
"Hali kwa wale wanaoishi hapa ni ya kutisha. Maeneo mengi hayafai tena kwa makaazi. Na kitu pekee kinachowapa baadhi ya watu faraja ni mshikamano mkubwa. Mshikamano pamoja na wale waliopoteza ndugu na marafiki, na ambao pengine bado hawajulikani waliko" amesema Kansela Merkel.
Ama kuhusu ujenzi na ukarabati wa miundombinu mikubwa ikiwemo barabara, madaraja na njia za reli, Kansela Merkel amekuwa muwazi na kuwatanabaisha wakaazi wa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kuwa hilo litachukua muda mrefu.
Ziara ya Merkel jimboni North Rhine Westphalia inafuatia ziara kama hiyo aliyoifanya siku ya Jumatatu katika jimbo jingine la Rhineland-Palatinate ambalo limeathiriwa zaidi na maafa ya mafuriko.
Wanasiasa walaumu Mabadiliko ya Tabianchi
Hadi sasa zaidi ya watu 160 wamekufa nchini Ujerumani na mamia wengine hawajulikani waliko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha wiki iliyopita na kusababisha mafuriko yaliyopasua kingo za mito, maji kufurika maakazi ya watu na kuharibu miundombinu.
Mafuriko hayo ambayo wanasiasa wa Ujerumani wameyanasibisha na athari za mabadiliko ya Tabianchi yamezua lawama kubwa ya umma kwamba serikali ilipwaya na mifumo ya tahadhari nchini Ujerumani haikusaidia chochote.
Katika taifa jirani la Ubelgiji ambalo nalo lilikumbwa na kadhia ya mafuriko wiki iliyopita, Mflame na Malkia wa nchi hiyo wameutembelea mji wa mashariki wa Verviers kutoa mkono wa pole kwa wale waliopoteza ndugu na jamaa au mali katika maafa hayo.
Zaidi ya watu 31 wamekufa nchini Ubelgiji na 70 wengine hawajulikani waliko tangu kiwango kikubwa cha maji ya mvua kilipovamia vijiji na miji ya mashariki wa taifa hilo.
Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo ametoa ahadi kwa wahanga kwamba serikali mjini Brussels haitawatelekeza.