Merkel atembelea kituo cha ujumbe wa Umoja wa Ulaya Niger
3 Mei 2019Maafisa wa ujumbe huo wa kujenga uwezo nchini Niger EUCAP Sahel , walizungumza na kansela kuhusu uhamiaji, ugaidi, uhalifu wa kupangilia, ulinzi wa kutumia magari katika mpaka na usafirishaji wa madawa ya kulevywa.
Ujumbe huo , ambao kwa sasa unafikia wafanyakazi 120 wa Umoja wa Ulaya na wafanyakazi kutoka katika mataifa ya eneo hilo, uliundwa na Umoja wa Ulaya mwaka 2012 kufanyakazi ya kutoa mafunzo kwa polisi ya Niger pamoja na maafisa wengine wa usalama ambao jukumu lao ni kupambana na ugaidi na uhalifu wa kupangilia katika kanda hiyo.
"Ningependa kwanza kuwashukuru kwa kuwa katika ujumbe huu, kwasababu kwanza ni maalum . Ujumbe huu ni mgumu na bila shaka ni wa hatari sana kwa jeshi la Ujerumani."
Kabla ya kurejea nyumbani mjini Berlin, Merkel alitarajiwa kufanya ziara katika shirika la kupigania haki za binadamu la wanawake lililoundwa mwaka 1998 kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya matumizi ya nguvu majumbani.
Merkel ametoa tuzo kwa ajili ya usawa wa jinsia iliyotolewa kwake na serikali ya Finland kwa shirika hilo, ambalo litatumia euro 150,000 za tuzo hiyo kujenga makaazi kwa wanawake mjini Niamey.
Ziara hiyo ambayo ilimfikisha pia nchini Burkina Faso na Mali ilimalizika leo mjini Niamey, ambapo serikali ya Ujerumani ilikuwa inataka kutumia ziara hiyo ya mataifa ya Afrika kama sehemu ya kulinyooshea mkono bara hilo kutokana na maafa baada ya mzozo wa uhamiaji.
Ujerumani yataka kusaidia ulinzi
Merkel amekwenda katika ziara hiyo akiwa na vivutio kadhaa kusaidia serikali ya rais wa Niger Mahamadou Issoufou, ili kuimarisha nchi yake yenye matatizo.
Miongoni mwa ahadi alizotoa ni pamoja na kupanua mpango wa kuwahamisha wakimbizi wa kutoka Eritrea na Somalia , mpango ambao unatekelezwa kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR.
Kama sehemu ya mpango huo, wakimbizi ambao wamekwama nchini Libya wanapelekwa nchini Niger , ambapo kutoka hapo wanapelekwa nchini Ujerumani.
Ujerumani pia inataka kusaidia maendeleo ya kijamii na kijeshi nchini Niger, msisitizo ukiwa katika kuleta hali bora ya utoaji wa huduma ya afya, mipango ya uzazi na elimu. Kansela pia amesisitiza ukweli kwamba kuleta hali bora ya usalama hakuwezi kufanikishwa kwa njia za kijeshi pekee.
Merkel alikwenda siku ya Alhamis nchini Mali akitokea Burkina Faso ambako alitetea sera ya Ujerumani ya kujizuwia kuyauzia silaha mataifa ya eneo hilo. Merkel amesema kuna hatari kwamba magaidi wanaweza kukamata silaha zilizoletwa kusaidia mataifa ya Afrika kupambana na ugaidi.