Merkel atetea uamuzi wa kupeleka silaha Iraq
1 Septemba 2014Akilihutbia bunge mjini Berlin baada ya kupitishwa uamuzi huo wa kupatiwa silaha wapiganaji wa Kikurdi nchini Iraq siku ya Jumapili, Kansela Merkel amesema ingawa anatambua hakuna mgogoro unaoweza kusuluhishwa kwa kutumia silaha, lakini kuna mazingira ambapo msaada wa kijeshi tu ndiyo unaweza kuhakikisha suluhu ya kisiasa inapatikana, na kuongeza kuwa hawawezi kunyamazia kitisho cha kundi la Dola ya Kiislamu.
"Uamuzi huu ni mpana. Tuliupima kwa umakini sana na kuainisha masuala kadhaa ya siasa ya nje na usalama. Tulikuwa na chaguo la ama kutochukuwa hatari, kutopeleka chochote na mwishowe tukubali kutanuka kwa ugaidi, au kuwasaidia wale wanaopambana kishujaa, kwa kidogo tunachoweza ili waweze kukabiliana na ukatili wa Dola ya Kiislamu. Tunafahamu juu ya hatari zinazoweza kutokana na msaada kama huo, na bila shaka tuliyazingatia yote hayo," alisema Merkel.
Wajerumani ndani ya IS
Serikali ya Ujerumani ilitangaza jana Jumapili kuwa itatuma vifaa vya kijeshi vikiwemo maroketi ya kushambulia vifaru, bunduki za kisasa na magruneti ya mkononi kwa Wakurdi wanaopambana dhidi ya kundi la Dola ya Kiislamu. Merkel amesema takribani raia 400 wa Ujerumani walikwenda nchini Iraq na Syria kupigana kwa upande wa wapiganaji wa jihadi, ambao amesema wanatishia utulivu wa kanda nzima.
Merkel amepinga tuhuma za upinzani kwamba silaha hizo huenda zikaangukia katika mikono isiyo sahihi, au kwamba Ujerumani ilikuwa inaelekea taratibu katika matumizi ya kijeshi, na kusema kinachoendelea hivi sasa ni kibaya zaidi kuliko kile ambacho kinaweza kutokea kutokana na kutolewa kwa silaha hizo.
Wizara ya Ulinzi imesema vifaa vya Ujerumani ambavyo vitawasilishwa kwa awamu tatu, vinahusisha mifumo 30 ya makombora ya kushambulia vifaru, bunduki 16,000 za mashambulizi bastola 8,000 na mitambo midogo ya kufyatulia maroketi.
Pmaoja na silaha, Ujerumani pia inapanga kutuma vifaa vingine kama vile mahema, kofia za chuma na vifaa vya mawasiliano. Shehena ya kwanza itaweza kuwawezesha kuwa na vifaa, wanajeshi wapatao 4,000 kufikia mwezi Septemba. Vifaa hivyo ambavyo vimetolewa katika hifadhi ya jeshi la Ujerumani, vinakadiriwa kuwa na thamani ya euro milioni 70.
Jeshi la Ujerumani pia linapanga kulileta kundi dogo la wapiganaji wa Pershmega wa Kikurdi kusini mwa Ujerumani kwa ajili ya mfunzo ya wiki moja kuhusiana na matumizi ya zana hizo.
Upelekaji silaha katika maeneo yenye migogoro siyo jambo la kawaida nchini Ujerumani, kutokana na historia yake katika vita viwili vikuu vya dunia, na imekuwa ikijuzuwia kushiriki operesheni za kijeshi nje ya nchi, na kisheria haipeleki silaha katika maeneo ya kivita.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpa,rtre
Mhariri: Saum Yusuf