Merkel atowa wito kupambana na umaskini Afrika
13 Juni 2017Kansela Merkel amesema "Ukosefu wa matumaini ni mkubwa mno barani Afrika hapo tena bila ya shaka kutakuwepo na vijana wanaoamini kwamba inabidi watafue maisha mapya mahala kwengine duniani.Kwa hiyo iwapo tutashirikiana na nyinyi kuzisaidia nchi zenu hapo tutakuwa pia tunajiletea usalama zaidi sisi wenyewe binafsi na tunaweza kukomesha watu wanaofaidika kinyume na sheria kwa masahahibu ya wengine."
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiufunguwa mkutano wa kundi la mataifa G20 lenye maendeleo ya kiuchumi na yale yanayoinukia kiuchumi duniani mjini Berlin hapo jana pamoja na viongozi 10 wa Afrika kama sehemu ya urais wa Ujerumani wa kundi la nchi hizo ambapo itakuwa na mkutano wake wa kilele mwezi ujao nchii Ujerumani.
Merkel amesema zaidi ya nusu ya Waafrika umri wao ni chini ya miaka 25 na idadi hiyo inatazamiwa kuongezeka maradufu kufikia katikati ya karne hii na kufanya ukuaji wa uchumi na ajira kuwa mambo muhimu sana.
Ujerumani yapokea zaidi ya watafuta hifadhi milioni moja
Ujerumani imepokea zaidi ya watafuta hifadhi milioni moja tokea mwaka 2015 wengi wao wakitokea Mashariki ya Kati bali pia maelfu wengine kutoka Ethiopia,Nigeria na mahala kwengineko barani Afrika.
Mamia kwa maelfu wamekuwa wakikimbia kupitia jangwa la Sahara kwa kupitia Libya nchi iliokosa utawala wa sheria kwa kutaraji kwamba wafanya biashara ya kusafirisha watu kwa mgendo watawafikisha barani Ulaya kwa kutumia mashua zilizochakaa.
Rais wa Cote d' Ivoire Allassane Oatarra amesema ufumbuzi uko katika kuzalisha ajira kwa wingi mkubwa kwa kupitia ukuaji wa kiuchumi imara na shirikishi.
Mkutano huo wa siku mbili mjini Berlin unawajumuisha viongozi wa Misri, Ghana,Cote d `Ivoire Mali,Niger,Rwanda ,Senegal na Tunisia halikadhalika Benki ya Dunia ,Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na Umoja wa Afrika.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Daniel Pulz
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman