Wakimbizi kupewa vitambulisho maalum Ujerumani
15 Januari 2016Peter Dreier, anayehusishwa na wapiga kura huru wa kundi la kisiasa jimboni Bavaria, alilileta basi lililojaa wakimbizi wa Syria walio kati ya miaka 21 na 45 katika safari ya kilomita 550 kutoka eneo la vijijini la Kusini Mashariki mwa mji wa Landshutl hadi katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin.
Muakilishi wa kamati ya seneti ya afya na masuala ya jamii walilikaribisha kundi hilo na kuwatafutia mahala pa kukaa kwa usiku mmoja kufuatia maagizo ya dharura yaliyotolewa kutoka ofisi ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Hata hivyo msemaji wa mji huo amesema wakimbizi hao walikataa pendekezo hilo na baadaye walipewa mahala pa kulala katika chumba kimoja cha kulala kaskazini mwa mji huo.
Kundi hilo halikuwa na paspoti lakini walikuwa wanatarajia kupata mahala pazuri pa kulala. Wakimbizi hao walitarajiwa kusafirishwa na kurejeshwa jimboni Bavaria hapo jana. Kufuatia tukio hilo mwanasiasa Peter Dreier alisema haoni mwisho wa wimbi la wakimbizi kuingia ujerumani lakini ukweli ni kwamba uwezo wa kutoa hifadhi kwa wakimbizi hao unapungua haraka, sababu haoni ujenzi wowote mpya wa nyumba zao.
Bunge la Ujerumani laridhia mpango wa vitambulisho vipya kwa wakimbizi
Aidha sera ya uhamiaji ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel imepinga katika nafasi za juu za maafisa wa muungano wake baada ya wakimbizi milioni 1.1 walipoingia Ujerumani mwaka wa 2015 ambapo wanasiasa kutoka chama chake ndugu cha Bavaria wakitaka kupunguzwa kwa idadi ya wakimbizi wanaoingia ujerumani mwaka wa 2016.
Huku hayo yakiarifiwa bunge la Ujerumani limeidhinisha mpango wa vitambulisho vipya kwa wakimbizi ambapo data au taarifa zao zitahifadhiwa katika mfumo wa serikali. Sheria hiyo mpya ambayo imeshaidhinishwa na baraza la mawaziri la Angela Merkel itasababisha kila mkimbnizi kupokea kitambulisho kimoja kitakachokuwa na taarifa zake zote, kama alama ya vidole, nchi anayotokea, habari juu ya afya yake na ujuzi aliyonao.
Vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa kuanzia mwezi wa Februari na mfumo huo mpya kutekelezwa kikamilifu nchi nzima kufikia kipindi cha kiangazi.
Hatua hii imenuiwa kuwafuatilia wakimbizi wanaozidi kuingia nchini Ujerumani, na inakuja baada ya ukosoaji dhidi ya mfumo wa kuhifadhi data kwa kila jimbo ambao unaruhusu baadhi ya wahamiaji kutoa taarifa zisizokuwa na ukweli ama kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Mwandishi Amina Abubakar/dpa
Mhariri Daniel Gakuba