Merkel autuliza mvutano ndani ya CDU kuhusu wakimbizi
15 Desemba 2015Ikiwa kulikuwa na kitu kilichojitokeza wazi kutokana na kitendo cha wajumbe kusimama na kumpigia makofi kwa dakika kadhaa Kansela wa Ujerumani, ni kuwa chama chake cha siasa za wastani za mrengo wa kulia kwa mara nyingine kimeungana na kusimama na kiongozi wake, angalau kwa sasa.
Merkel aliyekuwa mwenye furaha jana alionekana kutuliza mvutano ndani ya kambi ya CDU na kujiokoa kutokana na wimbi jipya la shutuma kuhusiana na namna anavyoushughulikia mgogoro wa wakimbizi – hasa kwa sababu ya azimio lililofikiwa na kamati kuu ya CDU katika mkesha wa mkutano mkuu wa chama.
Mswada huo, ambao umewasilishwa kwa wajumbe wa chama katika mkutano huo unaokamilika leo, unasema kuwa chama kinadhamiria kupunguza idadi ya wakimbizi wanaoingia Ujerumani “kupitia hatua mwafaka”, lakini unaepuka kutaja “ukomo wa juu” kama wanavyotaka wakosoaji wa Kansela.
Wajibu wa kiutu
Merkel aliwaambia karibu wajumbe 1,000 wa CDU kuwa serikali yake inadhamiria kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wakimbizi wanaowasili Ujerumani. "Tunahitaji, kama ilivyo katika azimio la Karlsruhe, suluhisho la mgogoro wa wakimbizi ambalo ni endelevu na la kudumu. Suluhisho ambalo linatimiza matakwa ya Ujerumani na Ulaya. Suluhisho ambalo linaweza kufanya kazi katika mshikamano wa Ulaya na kwa ushirikiano wa karibu na nchi wanakotoka na zinazotumiwa kama vituo vya muda kwa wakimbizi. Ni changamoto ya kimataifa, na inapaswa kutatuliwa kwa njia mwafaka ili kupata suluhisho la kudumu na endelevu".
Kiongozi huyo wa CDU amesema kama nchi yenye nguvu kubwa kiuchumi Ulaya, Ujerumani bado ina jukumu la “kimaadili na kisiasa” kuendelea kutoa msaada kwa watu waliokata tama na wanaoishi katika mazingira magumu kabisa duniani. ''Tutatimiza wajibu huo wa kiutu'', Alisema.
Kuhusiana na mswada huo, kiongozi wa tawi la vijana katika CDU Paul Ziemiak, aliondoa pendekezo la vijana la kuwekwa ukomo wa juu kwa waomba hifadhi Ujerumani, hata ingawa azimio hilo halitimizi sana mambo ambayo vijana wa CDU walitarajia.
Mwanachama wa bodi ya wanawake ya CDU na mjumbe wa jimbo la NRW Bianca Seeger aliisifu hotuba ya Merkel. Amesema Kansela ameangazia “masuala yanayoiathiri Ujerumani kwa sasa na matakwa ya watu wa Ujerumani”.
Huku idadi ya wakimbizi wanaoingia Ujerumani ikikaribia milioni moja, changamoto kubwa bado ipo, hasa wakati jamii ya Ujerumani ikijitahidi kuwashirikisha wageni wake wapya. Lakini kwa sasa, Merkel anaweza kupumua akifahamu kuwa juhudi zake za hapo jana zimeanzisha upya mshikamano ndani ya chama chake.
Mwandishi: Kate Brady/Bruce Amani/DW
Mhariri: Gakuba Daniel