Merkel na Chahed wazungumza ka kina
14 Februari 2017Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amependekeza kutoa fedha na vivutio vya elimu kwa watunisia watakaokuwa tayari kurudi kwa khiyari nchini mwao kama sehemu ya juhudi zake za kutaka kupunguza wimbi la wahamiaji wanaoingia nchini Ujerumani kutoka nchi za Kaskazini mwa Afrika.Wazo hilo la Kansela Angela Merkel limefuatia mkutano wake na waziri mkuu wa Tunisia aliyeko ziara mjini Berlin Yousef Chahed.
Kansela Angela Merkel amesema wamajediliana na waziri mkuu Chahed mapendekezo ya kuimarisha mipango ya elimu kwa ajili ya watunisia na kutoa fursa ya kuwapa fedha wale watakaokubali kuondoka kwa khiyari nchini Ujerumani na kwenda kuanzisha biashara nyumbani Tunisia. Hata hivyo mapendekezo ya Merkel yatajadiliwa zaidi na mawaziri wanaoziwakilisha nchi hizo mbili katika siku za hivi karibuni.
Pendekezo la Merkel
Mkutano wa Merkel na Chahed umekuja katika wakati ambapo mwishoni mwa juma Kansela huyo alidokeza fikra ya kutaka kuanzishwe kambi Afrika Kaskazini ya kuwapokea wakimbizi kama sehemu ya mpango wa kupunguza wimbi la wakimbizi wanaoingia Ulaya.Waziri mkuu Chahed lakini ameikataa fikra ya kutaka nchi yake Tunisia kuanzisha vituo vyake binafsi vya kuwapokea watu wanaoomba hifadhi ili kuipunguzia mzigo wa wakimbizi Ulaya.mapungufu katika mfumo huo yalionekana tangu mwezi Desemba baada ya kushindwa kurudishwa kwao mfuasi wa kundi la itikadi kali la dola la kiislamu raia wa Tunisia Anis Amri ambaye kimsingi alikuwa katika orodha ya watu wanaofuatiliwa nyendo zao na pia alikuwa ameshanyimwa hifadhi nchini Ujerumani miezi sita kabla ya kufanya mashambulizi ya kigadi na kuuwa watu 12 kwa kulivurumisha lori katika soko la Krismasi.
Katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Bild la Ujerumani waziri mkuu Chahed amesema ushirikiano na Ujerumani kuhusu suala la waomba hifadhi ulikuwa ukiendelea vizuri. lakini kwa mtazamo wake tatizo kubwa kwa Ulaya ni wakimbizi wanaotokea Libya kwenye Itali na hapo ndipo anaposhauri kwamba serikali ya Ujerumani inahitaji kufuata njia sahihi za kujaza nyaraka zinazotakiwa ili iweze kuwarudisha nchini Tunisia wakimbizi walionyimwa hifadhi ambao ni raia wa Tunisia.
Katika suala la kijana Anis Amri hatua ya kurudishwa kwao Tunisia ilichelewa kwa kisi kikubwa katika kupatikana nyaraka sahihi zilizotakiwa ikiwemo vitambulisho hali ambayo iliweka kipingamizi katika kurudishwa kwao.Alipigwa risasi na kuuwawa na polisi wa Italia mjini Milan mnamo tarehe 23 mwezi Desemba.Kwa maana hii waziri mkuu wa Tunisia amesema wahamiaji haramu wanaotumia nyaraka za uwongo wakati mwingine wanayafanya mambo kuwa magumu sana na kusababisha mchakato mzima kuchukuwa muda mrefu.
Lakini alipoulizwa juu ya ikiwa nchi yake iko tayari kujenga vito vya kuwapokea wakimbizi kwa msaada wa Ulaya waziri mkuu Chahed alisema nchi yake ni changa kidemokrasia na hafikiri kwamba hatua hiyo itafanya kazi na juu ya hilo Tunisia haina uwezo wa kujenga makambi ya wakimbizi ingawa kwa upande mwingine amesema mwelekeo zaidi unapaswa kuelekewa katika kupatikana suluhisho kwa Libya.Kwa upande wa Kansela Angela Merkel amedhoofishwa na sera yake ya kuiachja milango wazi kwa wakimbizi ambayo ilisababisha zaidi ya wakimbizi milioni moja kuingia nchini Ujerumani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.Sasa anajaribu kuwaonesha wapiga kura nchini Ujerumani kwamba anaimarisha usalama na kukabiliana na wakimbizi wasiotakiwa kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwezi Septemba mwaka huu.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman