1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel awataka Wajerumani kutochukia wageni

Mohammed Khelef31 Desemba 2014

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametumia hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2015 kuyakosoa maandamano yanayopinga wageni na kuwalaumu viongozi wanaoyaratibu kwa kuwa na chuki nyoyoni.

Kansela Angela Merkel akihutubia taifa kuuaga mwaka 2014 na kuukaribisha 2015.
Kansela Angela Merkel akihutubia taifa kuuaga mwaka 2014 na kuukaribisha 2015.Picha: Reuters/Maurizio Gambarini/Pool

"Wanaposema sisi ndio watu, wanachomaanisha hasa ni kwamba nyinyi wengine si wa hapa kwa sababu ya rangi za ngozi zenu au dini zenu. Hivyo wacha nimwambie kila anayeshiriki maandamano hayo kwamba usifuate wito wao, kwa sababu sehemu kubwa ya kile kilichomo nafsini mwao ni dharau, ukatili na hata chuki," alisema Kansela huyo.

Hotuba hii ya aina yake ya Kansela Merkel inakuja huku kundi linalojiita Pegida, yaani Wazalendo wa Kizungu dhidi ya Kusilimishwa kwa Bara la Ulaya, likiwa limeshafanya maandamano kadhaa ya kila wiki, katika mji wa mashariki wa Dresden, wakiwakataa Waislamu nchini Ujerumani.

Maandamano yao ya mwisho yaliyofanyika tarehe 22 Disemba, yalikusanya wafuasi 17,500, huku polisi ikisema takribani thuluthi moja ya Wajerumani wanakubaliana kwa kiasi fulani na maandamano hayo.

Kansela Merkel amesema Ujerumani ina wajibu wa kuwapa hifadhi watu wanaokimbia vita makwao na kuwapa nafasi ya kuwakuza watoto wao bila khofu.

"Moja ya matokeo ya vita na migogoro hii ni kwamba duniani kote kuna wakimbizi wengi zaidi hivi sasa kuliko ilivyowahi kuwa tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia. Wengi wanakimbia mauti. Kwa hivyo, ni jambo lisilo mjadala kwamba lazima tuwasaidie na kuwachukuwa wale wanaoomba hifadhi kwetu." Alisema Kansela Merkel akielezea kwamba Ujerumani imeshachukuwa waomba hifadhi 200,000 ndani ya mwaka jana pekee, ambao wamekuja kwenye taifa hili lenye nguvu kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya kunusuru maisha yao.

Maandamano ya kupinga Uislamu mjini Bonn, Bogida, tarehe 22 Disemba 2014.Picha: DW/Greta Hamann

Kwa kiasi fulani historia mbaya ya utawala wa Kinazi, sheria za kuomba hifadhi nchini Ujerumani ni za kiliberali zaidi kuliko mataifa mengi ya magharibi, kwani Wajerumani wenyewe walikubaliwa hifadhi kwenye mataifa kadhaa wakati wakipambana na utawala huo.

Matokeo yake ni kuwa suala la uhamiaji limekuwa zaidi kuwa ajenda ya kisiasa kuliko ya kibinaadamu. Baadhi ya wanachama wa vyama vya kihafidhina wanahofia kupoteza uungaji mkono wa wapigakura ikiwa hawatabadilisha mtazamo wao kuakisi matakwa ya wapigakura hao.

Mzozo wa Ukraine

Kuhusiana na mzozo wa Ukraine, Kansela Merkel amesema kujiingiza kwa Urusi kwenye mzozo huo ndani ya mwaka jana yalikuwa majaribu makubwa kwa misingi ya amani barani Ulaya.

Wajerumani wakifuatilia hotuba ya Kansela Merkel kwa njia ya televisheniPicha: Reuters/Maurizio Gambarini

"Hakuna tone la shaka kwamba tunataka usalama barani Ulaya kwa kushirikiana na Urusi, na sio dhidi ya Urusi. Lakini pia Ulaya haiwezi kukubali na kamwe haitakubali ubabe wa mwenye nguvu zaidi kuzivunja sheria za kimataifa."

Kwa hilo, Kansela Merkel alitoa wito wa kuendelea kwa umoja miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya katika kukabiliana na Urusi kwa namna ambavyo mwaka 2014 ulidhihirisha.

Mara kadhaa, Ujerumani imesema kuwa kitendo cha Urusi kuuchukuwa mkoa wa Crimea kutoka Ukraine kilikuwa kinyume cha sheria na imetoa ushahidi unaoihusisha Urusi na kuwasaidia waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine, tuhuma ambazo Urusi inazikataa. Merkel amesema kuungana pekee hakutoshi, bali lazima kufuatiwe na kuchukuwa hatua:

"Kuungana pamoja sio lengo lenyewe, bali ndio ufunguo wa kuushindsa mzozo wa Ukraine na kusimamisha ukuu wa sheria."

Masuala mengine muhimu

Kansela Merkel ametumia pia hotuba hiyo ya kuuaga mwaka 2014 na kuukaribisha 2015 kugusia masuala mengine kadhaa ya kidunia na ya ndani, miongoni mwao ukiwa mripuko wa ugonjwa wa Ebola magharibi ya Afrika:

Wafanyakazi wa afya wakiwa kwenye operesheni ya kukabiliana na Ebola nchini Liberia.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

"Mwaka 2014 utasalia kwenye kumbukumbu zetu kama mwaka wa mripuko wa maradhi mabaya kabisa yaliyowakumba watu wa Afrika Magharibi. Ninawashukuru wale wote waliochangia kwenye kupambana na maradhi haya: madaktari, wauguzi, wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu na pia wanajeshi, waliojitolea maisha yao kwa ajili yetu."

Kansela Merkel pia amezungumzia kuibuka kwa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq, ambalo amesema linawauwa kikatili wale wanaopinga kukubaliana na utawala wake.

Amelitaja suala la kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya raia wa Ujerumani wanaozeeka kuwa changamoto kubwa inayoikabili nchi hii kwa sasa, akililinganisha na suala la kuingia wahamiaji kuwa ni jambo lenye faida kwa Ujerumani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters/AFP
Mhariri: Mohamed Dahman