Merkel azuru Uhispania baada ya makubaliano ya wakimbizi
12 Agosti 2018Akizungumza baada ya kuwasili siku ya Jumamosi katika mji wa San Lucar de Barrameda kusini mwa Uhispania kwa mazungumzo na waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, Pedro Sanchez , Merkel amesema kwamba Uhispania ilikuwa inaongoza majadiliano na nchi jirani yake ya Afrika kaskazini.
Ushirikiano wa ukweli na mataifa ya Afrika ni muhimu kuweza kupata kurejeshwa kwa waombaji hifadhi ambao wamekataliwa, aliongeza.
Uhispania , "imo katika mbinyo mkubwa wa wakimbizi wanaotoka katika mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara," Sanchez amesema.
Merkel ameongeza kwamba makubaliano na mataifa ya Afrika ya wanakotoka wakimbizi pamoja na nchi wanakopitia yatafanya kazi "pale tu wakati pande zote mbili zitakapopata kitu kutokana na hali hiyo, tunaweza tu tukazungumza kuhusu Afrika, tunapaswa kuzungumza na Afrika," amesema.
Sanchez na mkewe, Begona Gomez, walimlaki Merkel na mume wake, Joachim Sauer, mapema mchana, mwanzoni mwa ziara ya siku mbili ambamo suala la uhamiaji linatarajiwa kuwa ajenda muhimu.
Siku ya Jumatatu, Ujerumani na Uhispania zilifikia makubaliano kuwarejesha Uhispania wahamiaji wanaowasili nchini Ujerumani katika muda wa masaa 48 iwapo bado wana maombi ya kuomba hifadhi ambayo hayajakamilika nchini humo.
Makubaliano na nchi nyingine za Ulaya
Uhispania ni nchi ya kwanza katika Umoja wa Ulaya kutia saini makubaliano kama hayo na Ujerumani.
Alipoulizwa iwapo makubaliano hayo ni ishara tu , kutokana na kwamba waombaji wachache wa hifadhi wanawasili nchini Ujerumani baada ya kuorodheshwa nchini Uhispania, Merkel alisema kwamba inaonesha, "kwamba Ujerumani na Uhispania zinaunga mkono suluhisho la Ulaya " katika suala la uhamiaji.
Merkel ana matumaini ya kupata makubaliano kama hayo na Ugiriki na Italia baada ya msuguano mkubwa kuhusu sera za uhamiaji na waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer ambao ulitishia kuiangusha serikali yake ya muungano mapema mwezi Julai.
Mzozo huo ulishuhudia Merkel akiahidi hatua ambazo waombaji hifadhi ambao tayari wameandikishwa kwingine katika mataifa ya Umoja wa Ulaya wakirejeshwa katika taifa ambalo walijiandikisha kwanza kuomba hifadhi.
Pamoja na uhamiaji, viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili mageuzi ya kiuchumi na fedha katika Umoja wa Ulaya , mkutano wa kilele wa hivi karibuni wa NATO na ulinzi katika Umoja huo.
Pia alipangiwa kufanya ziara katika mbunga ya taifa iliyoko karibu na hapo ya Donana, kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Ujerumani siku ya Jumamosi. Kwa mujibu wa tarakimu kutoka katika shirika la kimataifa la uhamiaji , Uhispania imekuwa lengo jipya la wahamiaji kutoka bara la Afrika. Wengi wao wanatoka Morocco kupitia ujia wa Gibraltar , karibu kilometa 14 tu katika eneo lake la karibu, ama katika bahari ya Alboran iliyoko katikati ya rasi ya Iberia na Afrika kaskazini.
Kuanzia Januari hadi mwishoni mwa Julai, zaidi ya watu 23,000 waliingia Uhispania kupitia bahari ya Mediterania , wastani wa mara tatu katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Jacob Safari