Merkel, Hollande waionya Uingereza
18 Desemba 2015Akizungumza baada ya mkutano huo mjini Brussels, rais Hollande alisema masuala mawili nyeti katika matakwa ya Uingereza, yalihusu upatikanaji wa mafao ya kijamii kwa wahamiaji kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya yanayofungamanishwa na kanuni ya uhuru wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, na pia suala la kwamba mataifa yaliyoko nje ya kanda inayotumia sarafu ya euro hayapaswi kuzuwia ushirikiano zaidi wa eneo hilo la sarafu ya pamoja.
Hollande alisema matakwa ya serikai ya Uingereza laazima yazingatie na yaende sawia na kanuni za mikataba iliyopo ya Umoja wa Ulaya. Alisema kunaweza kuwepo na marekebisho na tahfifu, lakini akasisitiza kuwa kanuni, sheria na mikataba ya Umoja wa Ulaya laazima iheshimiwe.
Pia akizunguma baada ya chakula cha usiku walichoshiriki pamoja viongozi wakuu wa mataifa ya Umoja wa Ulaya, kansela wa Ujerumani Angela Merkel, alisema itakuwa vigumu kutimiza matakwa ya Uingereza ya kubadilisha sheria za Umoja wa Ulaya kuhusu mafao kwa wahamiaji, lakini akaongeza kuwa upo utashi miongoni mwa mataifa wanachama kufikia makubaliano.
"Nilieleza wazi kabisaa kwamba tuko tayari kulegeza msimamo lakini tutafanya hivyo kwa msingi wa kulinda kanuni za msingi za Ulaya, ambazo zinajumlisha kutobaguna na uhuru wa kusafiri," alisema Kansela Merkel.
Matumaini ya muafaka
Katika hotuba yake ndefu zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano ya kuhudhuria mikutano ya kilele ya Umoja wa Ulaya, waziri mkuu David Cameron aliwambia viongozi wengine 27 wa mataifa ya umoja huo kwamba ikiwa wanataka kuibakiza Uingereza katika Umoja wa Ulaya, laazima washughulikie malalamiko ya wapigakura wake kuhusu kudhibiti uhamiaji. Baada ya mkutano huo w ausiku, Cameron amesema leo kuwa anaona njia ya kufikia makubaliano.
"Ninachoweza kusema ni kwamba kuna njia ya kufikiwa makubaliano mwezi Februari. Itahitaji kazi kubwa lakini nilichohisi usiku wa leo kwenye chumba cha mkutano ni ishara nyingi za nia njema, watu wanataka makubaliano yatakayoibakiza Uingereza katika Umoja wa Ulaya kwa kutupatia fursa hiyo kwenye kura yaetu ya maoni. Lakini mengi yanapaswa kufanywa kati ya leo na wakati huo."
Viongozi wengine walioshiriki katika siku hiyo ya kwanza wa mkutano huo wa kilele walisema wanataka kumsaidiaCameron kuhakikisha kuwa taifa hilo lenye uchumi wa pili kwa ukubwa barani Ulaya na moja ya dola kubwa zaidi kijeshi lnasalia kwenye umoja huo. Lakini wengi walisisitiza kwamba suala la mabadiliko katika mikataba ya Umoja wa Ulaya halina mjadala.
Viongozi hao pia walikubaliana kuharakisha uundwaji wa kikosi cha ulinzi wa mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya, na kuhimizana kutekeleza hatua zilizokubaliwa mwaka huu kupunguza uhamiaji wa kuvuka bahari ya Mediterrani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae,
Mhariri: Saumu Yusuf