1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Hollande wamkalia kooni Putin

20 Oktoba 2016

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wamemkosoa rais wa Urusi Vladmir Putin kutokana na mashambulizi nchini Syria na wamekataa kuondoa uwezekano wa kuiwekea vikwazo Urusi.

Deutschland | AMerkel und Hollande Pressekonferenz zum Ukrainekonflikt im Kanzleramt
Picha: REUTERS/H. Hanschke

"Kinachotokea mjini Aleppo ni uhalifu wa kivita, moja ya matakwa ya kwanza ni kwamba mashambulizi ya utawala na waungaji wake mkono (Urusi) laazima yakome," alisema rais wa Ufaransa Francoise Hollande baada ya mkutano kati ya viongozi watatu mjini Berlin.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alilaani mashambulizi ya angani dhidi ya mji huo wa pili nchini Syria na kuyataja kuwa ya "kinyama na kikatili."  Viongozi wote wawili walionya kuwa hawataondoa uwezekano wa kuiwekea Urusi vikwazo, saa kadhaa kuelekea mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, ambako ushiriki wa Urusi nchini Syria utajadiliwa.

Kitisho cha vikwazo

"Kila kitu kinachoweza kuwa kitisho kinaweza kuw ana manufaa," Hollande alisema katika mkutano wa waandishi wa habari, wakati Merkel akiongeza kuwa "hatuwezi kuondoa njia hii." Akizungumzia mpango wa usitishaji mashambulizi ulioanza Alhamisi asubuhi, Hollande alisema Putin alionekana tayari kuurefusha mpango huo, uliopangwa kudumu kwa masaa 11, suala lililothibitishwa na hata Putin mwenyewe.

"Tumeweka wazi nia yetu ya kurefusha kadiri iwezekanavyo, kutegemeana na hali iliyopo ndani, usitishaji katika mashambulizi yetu," Putin alisema wakati wa mkutano wa habari uliotangazwa mojoa kwa moja na Televisheni ya Urusi.

Rais wa Urusi Vladmir Putin akihutubia mkutano wa waandishi habari mjini Berlin.Picha: REUTERS/A. Schmidt

Jeshi la Syria lilisema usitishaji huo mapigano ungedumu kwa siku tatu. Mji wa Aleppo unaoshikiliwa na waasi waliodhamiria kumuondoa madarakani rais Bashar Al-Assad, umekumbw ana mashambulizi makali zaidi tangu jeshi linalosaidiwa na Urusi lilipotangaza operesheni ya kuukomboa kikamilifu mwezi Septemba.

Mashambulizi ya angani yamesambaratisha kabisaa majengo na nyumba kadhaa za makaazi na miundombinu ya kiraia, katika kampeni ambayo Umoja wa Ulaya unasema inaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Muafaka kuhusu Ukraine

Kuhusu Ukraine viongozi hao walikubaliana juu ya ramani inayonuwia kufufua mchakato wa amani uliyokwama, ingawa maelezo y akina ya mpango huo bado yanahitaji kufanyiwa kazi na mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa hayo katika mwezi ujao.

Mpango huo ni sehemu ya juhudi za utekelezaji wa kile kinachoitwa makubaliano ya Minsk ya Februari 2015 kuhusu kumaliza mgogoro wa mashariki mwa Ukraine, ambamo zaidi ya watu 9,600 wameuawa

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alisema makubaliano yalifikiwa kwamba ichorwe ramani kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba, ambayo itahusisha masuala yaote, ikwemo kurejesha udhibiti wa Ukraine katika mpaka wake wote na Urusi.

"Pande zote zimekubaliana juu ya kuondolewa kwa vikosi vya Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi kutoka maeneo mapya manne katika uwanja wa mapigano katika mkoa wa Donbass. Tumeitetea ramani katika suala hilo. Ni ishara nzuri kwamba mazungumzo bado yanaendelea, alisema Poroshenko baada ya kutoka mkutanoni.

Mjadala juu ya uchaguzi Donbass

Poroshenko pia alinukuliwa akisema kuwa makubaliano yalifikiwa juu ya kupelekwa ujumbe wa polisi wenye silaha katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi wanaotaka kujitenga.

Lakini Merkel aliwaambia waandishi habari kuwa hatua kama hiyo itahitaji kwanza Ukraine ipitishe sheria za uchaguzi wa serikali za mitaa katika maeneo yanayogambaniwa, jambo ambalo Kiev bado haijalifanya.

Rais Poroshenko alisisitiza kuwa ataitisha uchaguzi katika mkoa wa Donbass pale tu vikosi vya kigeni vitakapoondoka.

Shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE lilisema mwezi Mei kuwa litafikiria kutuma ujumbe kusaidia kuendesha uchaguzi katika maeneo ya wanaotaka kujitenga.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko.Picha: REUTERS/M. Schlicht

Makubaliano ya Minsk

Makubaliano ya Minsk ya 2015 yalioratibiwa na Ufaransa na Ujerumani yamesaidia kumaliza mapigano ya kiwango kikubwa kati ya wanajeshi wa Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga, lakini makabiliano yameendelea na juhudi za kupata muafaka wa kisiasa zimekwama.

Uamuzi wa kuufanyia mkutano huo mjini Berlin umefuatia mfululizo wa diplomasia ya kwenye simu katika kipindi cha wiki iliyopita.

Nje ya ofisi ya kansela, mamia ya waandamanaji walifanya mikutano wakati viongozi hao wanne wakiwasili, likwemo kundi la watu 30 waliokuwa wakipeperusha bendera za Urusi na muungano wa Kisovieti na kuimba "ahsante Putin."

Karibu na hapo makundi makubwa ya waandamanaji wa Ukraine na Wasyria waliandamana dhidi ya rais huyo wa Urusi.

Putin alikuwa hajaizuru Ujerumani tangu Urusi ilipoitwa kimabavu rasi ya crimea kutoka kwa Ukraine mwaka 2014, na kusababisha kushuka uhusiano kati yake na mataifa ya magharibi kwa kiwango cha chini kabisaa tangu enzi za vita baridi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga

Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW