Merkel : Jumamosi ni siku ya maamuzi ya mzozo wa Ugiriki
26 Juni 2015Kufuatia siku ya kwanza ya Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya unaoendelea mjini Brussels Ubelgiji Merkel amesema mapema leo hii kwamba mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya inabidi waendelee na juhudi zao siku zinazokuja kwa sababu muda ndio huo unayoyoma.
Amesema viongozi wote wanaunga mkono wazo kwamba inapaswa kufanyika juhudi zote za kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Ugiriki kufikia Jumamosi.
Merkel amekaririwa akisema "Kuhusiana na mazungumzo na Ugiriki tumekubaliana kwamba kazi inabidi iendelee na taasisi tatu za mikopo na kwamba mkutano wa kundi la sarafu ya euro hapo Jumamosi utakuwa na umuhimu mkubwa sana wa kuamuwa kwa sababu muda unayoyoma.Tungelipenda mawaziri wa fedha na kundi la sarafu ya euro pamoja na taasisi hizo tatu na Ugiriki wafikie makubaliano na shauku hiyo imeelezwa bayana leo hii."
Kauli hiyo ya Merkel inakuja baada ya kushindwa tena kwa duru ya mazungumzo ya kanda ya sarafu ya euro hapo Ahamisi. Nchi 19 zinazotumia sarafu hiyo ya pamoja zimeshindwa tena kufikia makubaliano ya kunusuru Ugiriki kufilisika na madeni ambapo nchi hiyo ilikuwa inataraji ingelipatiwa mkupuo mwengine wa mkopo uliobakia wa euro bilioni 7.2 na Shirika la Fedha la Kimataifa.
Kutoka kwa Ugiriki Umoja wa Ulaya
Ugiriki inahitaji mikopo ya kulipa deni lake la euro bilioni 1.7 kwa IMF kufikia Juni 30.Kushindwa kufanya hivyo kutapelekea kufilisika kwa nchi hiyo jambo ambalo wachambuzi wanahofia kutailazimisha nchi hiyo kutoka kwenye kanda ya sarafu ya euro na pengine hata Umoja wa Ulaya.
Kutoka kwa Ugiriki kwenye kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya kutakuwa hakuepukiki iwapo serikali ya nchi hiyo na wakopeshaji wake watashindwa kupata ufumbuzi wa mzozo wa madeni wa Ugiriki katika kipindi cha siku tano.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Ujerumani Guenther Ottinger amesema watafanya kila wawezalo hadi hapo tarehe 30 Juni ili kwamba Wagiriki waonyeshe kuwa wako tayari kufanya mageuzi.
Madai ya ajabu
Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varaoufakis amesema nchi yake imefanya kila iwezalo kutimiza kile alichokiita "madai ya ajabu" yaliyotolewa na wakopeshaji wake na kwamba imeazimia kuendela kubakia kuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya.
Lakini amesema Ugiriki haitokubali ufumbuzi wa mzozo wake wa madeni ambao inauona kuwa hauna manufaa.
Akiandika kwenye mtandao wa Twitter mapema Ijumaa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Donald Tusk amefuta uwezekano wa kufanyika kwa mkutano maalum wa kilele wa viongozi wa kanda ya sarafu ya euro kama ule aliouitisha Jumatatu.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/DW
Mhariri : Iddi Ssessanga