1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kama Thatcher

28 Juni 2012

Magazeti ya Ujerumani leo (28.06.2012) yanazungumzia taswira ya Kansela Angela Merkel duniani kutokana na ushiriki wake kwenye mgogoro wa sarafu ya euro na pia siasa za ndani za Ujerumani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture alliance/dpa

Mhariri wa gazeti la Oldenburgische Volkszeitung linazungumzia taswira ya Kansela Angela Merkel katika vyombo vya habari vya mataifa mengine, wanachama wa kanda ya euro, akisema Kansela huyo ana "maadui wengi lakini pia ana heshima kubwa.

Vyombo vya habari katika nchi jirani vinamchukulia Kansela huyo kama mwanamke hatari na mwenye nguvu sana barani Ulaya. Mhariri anasema vyombo hivyo vinaweza kuwa viko sahihi, maana baada ya kuondoka madarakani kwa waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Margaret Thatcher, hakujawahi kuwa na mwanamke mwengine mwenye nguvu anayeweza kuitwa jina la Bibi wa Chuma, kama alivyoitwa Thatcher, ila yeye Kansela Merkel.

Na ulinganishaji huo umesadifu kuwa wa kweli, anasema mhariri. Kwa Merkel, kama ilivyokuwa kwa Thatcher, “hapana” inamaanisha “hapana”. Anamalizia mhariri kwa kusema kuwa Kansela Merkel anaibeba sera yake ya Ulaya kwa ukali, japo akiwa na heshima na tabasamu usoni. Akiwa na mkato wake wa nywele usiojali urembo, Kansela Merkel kutwa yuko kiguu na njia, nchi kwa nchi, akipeana mikono na kiongozi huyu, akibuasiana shavuni na yule, lakini akisimamia msimamo wake wa kuikoa euro isizame.

Euro yataka viongozi imara zaidi

Tugeukie sasa gazeti la Westdeutsche Allgemeine, ambalo linazungumzia mgogoro huo huo wa sarafu ya euro, lakini kwa pendekezo la mwenyekiti mteule wa chama cha Kansela Merkel, CDU, kwa jimbo la North-Rhine Westphalia, Armin Laschet.

Kansela Angela Merkel na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.Picha: Reuters

Anachosema Laschet ni kuwa “mgogoro wa euro unahitaji kuwa na mawaziri wa fedha imara na wabunge madhubuti wa Ulaya, maana watu walipoamua kujiingiza kwenye umoja wa sarafu hiyo, walitaka kuwa na nguvu za matumizi na sio nguvu za madeni.

Anachokipigania hasa, Lauschet, kwa mujibu wa mhariri wa Westdeutsche Allgemeine Zeitung, ni kuwa na Umoja wa Ulaya wenye nguvu zaidi ulivyo sasa, ambapo serikali husika zitayapeleka baadhi ya madaraka yake mengine kwa Umoja huo.

Kilio kwa wanajeshi wastaafu

Ikiwa mtu anadhani wanajeshi wastaafu wanaoishi maisha ya kidhalilifu ni Afrika tu, basi mkuu wa chama cha FDP kwenye Bunge la Ujerumani, Helmut Könighaus, anaweza kumstaajabisha na kilio chake, pale aliponukuliwa na gazeti hilo la Rheinische Post akisema kwamba hadhani ikiwa wanajeshi wastaafu wanapatiwa hata huduma za msingi, hasa katika mahitaji yao ya muda mrefu.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maizière.Picha: Jörg Enters/DGAP

Matokeo yake, maradhi ya kisaikolojia – kama vile mfadhaiko – yanakuwa ndiyo mwenza wao wa maisha, baada ya miaka kadhaa ya operesheni za kuilinda na kuijengea heshima nchi yao. Anachotaka sasa Könighaus ni kwa wastaafu hao kupatiwa huduma kamili, na maalum, zinazothamini nguvu na moyo wao wa kujitolea, kwa mujibu wa Rheinische Post.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Oldenburgische Volkszeitung, Westdeutsche Allgemeine, Rheinische Post
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW